Raia wauawa nchini Yemen, UN yataka ukweli kuhusu tukio hilo

8 Aprili 2019

Ripoti kutoka mji mkuu wa Yemen, Sana’a, zinasema kuwa raia 11 wakiwemo wanafunzi watano wameuawa ilhali wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio la Jumapili kwenye wilaya ya Shu’aub mjini humo.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Lise Grande amesema mashambulio hayo hayana maana na yanasababisha vifo na majeruhi  na ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa.

Akinukuliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa dharura, OCHA, Bi. Grande amesema kila juhudi zinapaswa kufanyika ili kufahamu mazingira yaliyosababisha vifo hivyo.

Amesema, “kulinda raia na miundombinu ya kiraia ni misingi mikuu ya sheria za kimataifa za kibinadamu,” na kwamba “hata kama tunahaha kushughulikia uhaba wa chakula ambalo ni janga baya zaidi la ukosefu wa chakula nchini duniani na moja ya milipuko mibaya zaidi ya ugonjwa wa kipindupindu, misingi hii ya sheria za kimataifa za kibinadamu bado inakiukwa.”

Mratibu huyo wa OCHA amesema watu ambao wako hatarini zaidi na wanahitaji msaada wa shirika hilo ndio hao hao ambao wanalipa gharama kubwa kwenye mzozo wa Yemen akisisitiza kuwa, “hili ni jambo baya kabisa.”

Kwa mujibu wa OCHA, wakati wa mwaka 2018, mashirika ya kibinadamu yaliripoti jumla ya matukio 45 ya mashambulio ya kijeshi kila wiki, maelfu ya raia wakiuawa mwaka jana ikiwemo zaidi ya watoto 950.

Mzozo wa Yemen umesababisha janga baya zaidi la kibinadamu ambapo takribani asilimia 80 ya wananchi wote miioni 24.1 nchini humo wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi.

“Watu milioni 10 wanakaribia kukumbwa na baa la njaa ilihali watu milioni 7 wanakabiliwa na utapiamlo,” imesema taarifa ya OCHA.

Ombi la mwaka huu wa 2019 la kusaidia Yemen n idola bilioni 4.2 kwa ajili ya watu zaidi ya milioni 20 lakini hadi leo ni asilimia 6 tu ya fedha hizo ndio zimepatikana.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter