Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bomu la kurushwa kutoka angani linahofiwa kuua wengi Yemen

Lango la wodi ya dharura katika Hospitali ya Dhamar, Yemen
UNOCHA Yemen
Lango la wodi ya dharura katika Hospitali ya Dhamar, Yemen

Bomu la kurushwa kutoka angani linahofiwa kuua wengi Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Taarifa ya pamoja iliyotolewa hii leo jumapili mjini Sana’a na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen pamoja na mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo imeeleza kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa takribani watu 60 wamefariki na wengine 50 kujeruhiwa katika eneo lililoko kaskazini mwa viunga vya mji wa Dhamar kwenye eneo ambalo awali lilikuwa chuo lakini sasa likitumika kama gereza linalokadiriwa kuwa na wafungwa 170.

 

Hata hivyo ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen imethibitisha kuwa wafungwa 52 ni miongoni mwa waliopoteza maisha na wengine takribani 68 haifahamiki waliko. Uwezekano wa waliofariki au kujeruhiwa kuongezeka ni mkubwa kwa kuwa juhudi za uokozi zinaendelea.

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yeman Bwana Martin Griffiths amenukuliwa akisema, “tukio la leo ni janga.Gharama za kibinadamu za vita hii ni hazielezeki. Tunahitaji kuzuia. Wayemen wanastahili mstakabali wa amani. Janga la leo linatukumbusha kuwa Yeman haiwezi kusubiri.”

Naye mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Yeman Bi Lise Grande amesema, “hili ni tukio la kutisha. Idadi ya waliojeruhiwa ni ya kushangaza. Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia ambazo leo zinaomboleza wapendwa wao.”

Waokoaji wa dharura wamekuwa wakihangaika kufikia katika eneo la tukio kutokana na kuendelea kwa mashambulizi katika eneo la tukio. Manusura bado wamekwama chini ya vifusi na juhudi za ukozi zinaendelea.

“Hizi ni nyakazi za kiza kwa Yemen,” ameeleza kwa masikitiko Bi Grande.

Naye Bwana Griffiths akarejerea wito akisema, “ni wazi, na tunasema tena na tena. Njia pekee ya kumaliza mauaji na shida nchini Yemen ni kumaliza mgogoro.”

Mgogoro wa kibinadamu wa Yemen ni mgogoro mbaya zaidi duniani kwa sasa ambapo takribani asilimia 80 ya watu wote yaani milioni 24.5 wanahitaji kwa namna fulani msaada wa kibinadamu na ulinzi.