Haki za watoto zinaendelea kusiginwa Palestina na kututia hofu kubwa-UN

1 Agosti 2018

Umoja wa Mataifa umesema unatiwa hofu kubwa na kuendelea kukiukwa kwa haki za watoto kwenye maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina, na kutaka hatua muhimu na za haraka kuchukuliwa ili kuruhusu watoto kuishi kwa uhuru bila hofu na kufurahia haki zao.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa hii leo, mratibu wa masuala ya kibinadamu katika eneo linalokaliwa la Palestina Jamie McGoldrick , mkuu wa ofisi ya haki za binadamu wa eneo hilo James Heena na mwakilishi maalumu wa shirikala Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwenye eneo la Palestina Genevieve Boutin wamesema, licha ya onyo na wito unaoendelea kutolewa na  Umoja waMataifa na wadau wengine kutoa kipaumbele kwenye ulinzi wa watoto, lakini bado wiki baada ya wiki taarifa zinazoibuka Gaza na maeneo mengine yanayokaliwa ya Palestina ni za watoto kuuawa na kujeruhiwa vibaya wakiwa umri wa miaka 11 tu.

Wakati huohuo wamesema watoto nchini Israel wanakabiliwa na hofu, athari za kisaikolojia na kujeruhiwavibaya. Kwa mwezi huu pekee watoto saba wa Kipalestina wameuawa kwa risasi na magruneti yanayovurumishwa kutoka Israel , huku wasichana wawili wa Kiisrael wenye umri wa miaka 14 na 15 wameripotiwa kujeruhiwa vibaya kutokana na makombora na magruneti yanayorushwa kuelekea Israel na makundi ya Kipalestina yenye silaha .

Watoto kwenye kambi ya wakimbizi wa Khan Younis, Gaza. Picha:UNICEF Palestina / Eyad El Baba
Watoto kwenye kambi ya wakimbizi wa Khan Younis, Gaza. Picha:UNICEF Palestina / Eyad El Baba

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wameongeza kuwa tangu Machi 30 mwaka huu watoto 26 wa Kipalestina wameuawa, 21 kati yao wakati wa maandamano na watano wengine wameuawa na magruneti yanayorushwa na Israel au nje ya maandamano. Na katika kipindi hichohicho mamia ya watoto wengine wamejeruhiwa na idadi kubwa ya watoto hawa watakuwa na vilema vya maisha ikiwa ni pamoja na kukatwa viungo vyao.

Kwa sasa Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watoto hawa wanahitaji msaada wa haraka wa kisaikolojia, huduma maalumu za afya, na ushauri nasaha. Wamesiitiza kuwa kila siku watoto hawa hususan wa Ukanda wa Gaza wanapokonywa haki zao, na sasa wametoa wito kwa Israel, Mamlaka ya Palestina pamoja na Hamas kuweka mslahi ya watoto mbele na kuchukua hatua za haraka kukomosha madhila hayo kwa watoto na hili sio chaguo ni wajibu.

TAGS: OCHA, UNICEF, Israel, Palestina, watoto , haki za binadamu

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter