Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukwepaji wa sheria Israel lazima ukomeshwe:Bachelet

Mazishi yaShirin Abu Akleh mjini Jerusalem
Maisa Abu Ghazaleh
Mazishi yaShirin Abu Akleh mjini Jerusalem

Ukwepaji wa sheria Israel lazima ukomeshwe:Bachelet

Haki za binadamu

Uchunguzi lazima ufanyike dhidi ya hatua zinazochukuliwa na vikosi vya usalama vya Israel, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet amesema Jumamosi, akitoa wito wa uwajibikaji na kukomeshwa kwa  tabia ya watu kutoadhibiwa.

Wito wake unakuja kufuatia mauaji ya mwandishi wa Habari wa Al Jazeera Shireen Abu Akleh, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano wiki hii alipokuwa akiripoti uvamizi wa Israel huko Jenin, kwenye Ukingo wa Magharibi.

Mwanahabari huyo mkongwe wa mmarekani mwenye asili ya Palestina alizikwa Jerusalem Mashariki siku ya Ijumaa na umati mkubwa wa watu ulijitokeza kwa ajili ya mazishi yake.

Matumizi ya nguvu kupita kiasi

Kamishna Mkuu ametoa taarifa akisema amekuwa akifuatilia kwa huzuni kubwa matukio yanayoendelea kwenye eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki.

"Picha za polisi wa Israel wakiwashambulia waombolezaji kwenye msafara wa mazishi ya mwanahabari Shireen Abu Akleh huko Jerusalem Mashariki siku ya Ijumaa tarehe 13 Mei zilishtua. Ripoti zinaonyesha kuwa takriban watu 33 walijeruhiwa," alisema kamishina huyo.

Bi Bachelet amesema matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na Israel, ambayo yalikuwa yakirekodiwa na kurushwa moja kwa moja, yanaonekana kuwa si ya lazima na lazima yachunguzwe haraka na kwa uwazi.

"Lazima kuwe na uwajibikaji kwa mauaji ya kutisha sio tu ya Shireen Abu Akleh lakini kwa mauaji yote na majeruhi mabaya katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu," amesema.

Wito wa kufanyika uchunguzi

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameripoti kuwa hadi sasa kwa mwaka huu pekee Wapalestina 48 wameuawa na vikosi vya usalama vya Israel.

Kifo cha hivi karibuni zaidi kilitokea Jumamosi wakati kijana mmoja aitwaye Walid al-Sharif, alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapigano mwezi uliopita katika eneo la msikiti wa Al Aqsa mjini Jerusalem.

"Kama nilivyotoa wito mara nyingi hapo awali, lazima kuwe na uchunguzi ufaao kuhusu vitendo vya vikosi vya usalama vya Israeli," amesema Bi Bachelet na kuongeza kuwa “Yeyote atakayebainika kuhusika achukuliwe hatua za kinidhamu na adhabu zinazolingana na uzito wa ukiukwaji huo wa haki za binadamu. Utamaduni huu wa kutokujali lazima ukomeshwe sasa.”

Baraza la Usalama la laani

Mauaji ya Bi Abu Akleh yameibua mshtuko kote ulimwenguni, na maafisa wa Umoja wa Mataifa wamekuwa miongoni mwa wanaotaka uchunguzi ufanyike.

Mwanahabari huyo alipigwa risasi ingawa alikuwa amevalia fulana iliyomtambulisha kama mwanachama wa kikosi cha waandishi wa habari. Mtayarishaji wake  wa vipindi pia alijeruhiwa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa taarifa Ijumaa likilaani vikali mauaji yake, na kurejea kusema kwamba waandishi wa habari wanapaswa kulindwa kama raia.

Baraza pia lilitoa wito wa uchunguzi wa haraka, wa kina, wa uwazi, na wa haki na bila upendeleo kuhusu mauaji yake, na kusisitiza haja ya kuhakikisha uwajibikaji.