Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Makaburi ya halaiki yaonesha waathirika walikuwa wamefungwa mikono - OHCHR

Watu wakiwa wamekusanyika nje ya Hospitali ya Al Shifa Gaza ambako kumepatikana makaburi ya halaiki
WHO
Watu wakiwa wamekusanyika nje ya Hospitali ya Al Shifa Gaza ambako kumepatikana makaburi ya halaiki

GAZA: Makaburi ya halaiki yaonesha waathirika walikuwa wamefungwa mikono - OHCHR

Haki za binadamu

Ripoti za kutisha zinaendelea kuibuka kuhusu makaburi ya halaiki huko Gaza ambako waathirika wa Kipalestina wameripotiwa kuvuliwa nguo wakiwa wamefungwa mikono, jambo ambalo limezusha wasiwasi juu ya uwezekano wa  kuweko kwa vitendo vya uhalifu wa kivita huku kukiwa na mashambulizi ya anga ya Israel yakiendelea kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR.

Hatua hiyo inafuatia kupatikana mwishoni mwa juma “kwa mamia ya miili  ya watu  iliyozikwa chini kabisa ardhini na kufunikwa na taka katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis, katikati mwa Gaza na katika Hospitali ya Al-Shifa katika Jiji la Gaza kaskazini. Jumla ya miili 283 iliopolewa katika Hospitali ya Nasser, na 42 kati yao ilitambuliwa.”

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo Ravina Shamdasani, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu amesema "Miongoni mwa waliofariki dunia walidaiwa kuwa wazee, wanawake na majeruhi, huku wengine wakipatikana wakiwa wamefungwa mikono yao na kuvuliwa nguo." 

Kilichobainika katika hospitali ya Al-Shifa

Akitoa mfano wa mamlaka ya afya ya eneo la Gaza, Bi. Shamdasani ameongeza kuwa miili zaidi imepatikana katika hospitali ya Al-Shifa.

Hospitali hiyo kubwa iliyokuwa kituo kikuu cha elimu ya juu cha eneo linalokaliwa la Ukanda wa Gaza kabla ya vita kuzuka tarehe 7 Oktoba mwaka jana  kwa lengo la uvamizi wa kijeshi wa Israel kuwaondoa wanamgambo wa Hamas wanaodaiwa kufanya operesheni ndani ambayo ilimalizika mwanzoni mwa mwezi huu. 

Baada ya wiki mbili za mapigano makali, wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa walithibitisha tarehe 5 Aprili kwamba Al-Shifa ilikuwa ganda tupu, na vifaa vingi vikiwa vimeteketea kabisa na kusalia majivu.

“Ripoti zinaonyesha kuwa kulikuwa na miili 30 ya Wapalestina iliyozikwa katika makaburi mawili katika ua wa Hospitali ya Al-Shifa katika Jiji la Gaza, moja mbele ya jengo la huduma ya dharura na jingine mbele ya jengo la huduma ya kusafisha figo,” amesema Bi Shamdasani akiwaambia waandishi wa habari mjini Geneva.

Miili ya Wapalestina 12 sasa imetambuliwa kutoka maeneo haya huko Al-Shifa, msemaji huyo wa OHCHR ameendelea kusema na kuongeza kuw lakini utambuzi bado haujawezekana kwa miili ya watu waliobaki.

"Kuna ripoti kwamba mikono ya baadhi ya miili hii pia ilikuwa imefungwa," amesema Bi. Shamdasani na kuongeza kwamba kunawezekana kuwa na "waathiriwa wengi zaidi licha ya madai ya jeshi la ulinzi la Israeli kuwaua Wapalestina 200 wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika katika hospital ya Al. -Shifa”.

Binti mdogo akiwa anasafirishwa kutoka hosptali ya Kamal Adwan Ksskazini mwa Gaza
© WHO
Binti mdogo akiwa anasafirishwa kutoka hosptali ya Kamal Adwan Ksskazini mwa Gaza

Siku 200 za jinamizi

Takriban siku 200 tangu mashambulizi makali ya Israel yaanze kulipiza kisasi mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ameelezea kusikitishwa kwake na uharibifu wa hospitali za Nasser na Al-Shifa na taarifa ya kugunduliwa kwa makaburi ya pamoja.

Akitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haraka kuhusu vifo hivyo Bwana Türk amesema "Mauaji ya makusudi ya raia, wafungwa, na wengine ambao si wanajeshi wapiganaji ni uhalifu wa kivita," 

Idadi ya vifo inaendelea kuongezeka

Kufikia Aprili 22, zaidi ya Wapalestina 34,000 wameuawa huko Gaza, wakiwemo watoto 14,685 na wanawake 9,670, ofisi ya Kamishna Mkuu imesema, ikiinukuu takwimu za mamlaka ya afya Gaza. 

Ameongeza kuwa watu wengine 77,084 wamejeruhiwa, na wengine zaidi ya 7,000 wanadhaniwa kufukiwa chini ya vifusi.

Kamishna Mkuu  amesema “Kila baada ya dakika 10 mtoto mmoja huuawa au kujeruhiwa. Watoto wanapaswa kulindwa chini ya sheria za vita, lakini bado wao ndio ambao wanalipa gharama kubwa katika vita hivi”.

Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na UN News
UN Photo/Mark Garten
Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na UN News

Onyo la Türk

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza onyo lake dhidi ya uvamizi kamili wa Israel huko Rafah, ambapo takriban watu milioni 1.2 wa Gaza wamelazimika kukimbilia na kupata hifadhi.

"Viongozi wa dunia wanasimama kwa umoja juu ya umuhimu wa kuwalinda raia walionaswa huko Rafah," amesema Kamishna Mkuu katika taarifa yake, ambayo pia imelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Rafah katika siku za hivi karibuni ambayo yaliwaua wanawake na watoto.

Hii ni pamoja na shambulio dhidi ya jengo la ghorofa katika eneo la Tal Al Sultan tarehe 19 Aprili ambalo liliua Wapalestina tisa "wakiwemo watoto sita na wanawake wawili pamoja na makombora kwenye Kambi ya As Shabora huko Rafah siku moja baadaye na kusababisha vifo vya watu wanne, wakiwemo msichana na mwanamke mjamzito.”

Ameendelea kusema kwamba "Picha za hivi punde za mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati wake au njiti aliyechukuliwa kutoka tumboni mwa mama yake anayekufa, na mashambulizi ya nyumba mbili zilizo karibu ambapo watoto 15 na wanawake watano waliuawa hii ni zaidi ya vita na ni ukatili usiokubalika." 

Kamishna Mkuu ameshutumu "mateso yasiyoelezeka yanayosababishwa na vita vya miezi kadhaa sasa na ameomba kwa mara nyingine tena maafa na uharibifu, njaa na magonjwa, na hatari ya migogoro mingi vikomeshwe.”

Familia Gaza ikipata mjo katika kifusi cha nyumba yao
© WFP/Ali Jadallah
Familia Gaza ikipata mjo katika kifusi cha nyumba yao

Bwana. Türk pia amesisitiza wito wake wa kusitisha mapigano mara moja, kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia waliochukuliwa kutoka Israel na wale wanaozuiliwa kiholela, na mtiririko usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu.

Mashambulizi makubwa ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi

Akigeukia Ukingo wa Magharibi, mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa amesema kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea huko "bila kupunguzwa".

Hii ilikuwa licha ya kulaaniwa kwa kimataifa kwa "mashambulizi makubwa ya walowezi kati ya tarehe 12 na 14 Aprili ambayo yaliwezeshwa na vikosi vya usalama vya Israeli ISF".

Vurugu za walowezi zimeandaliwa "kwa msaada, ulinzi, na ushiriki wa ISF", amesema Türk alisisitiza, kabla ya kuelezea operesheni ya muda mrefu ya saa 50 katika kambi ya wakimbizi ya Nur Shams na mji wa Tulkarem kuanzia tarehe 18 Aprili.

"ISF ilipeleka askari wa ardhini, tingatinga na ndege zisizo na rubani na kufunga kambi hiyo. Wapalestina kumi na wanne waliuawa, watatu kati yao wakiwa ni watoto,” mkuu huyo wa haki za Umoja wa Mataifa amesema, akibainisha kuwa wanachama 10 wa ISF pia wamejeruhiwa.

Katika taarifa yake Bwana Türk pia ameangazia ripoti kwamba Wapalestina kadhaa waliuawa kinyume cha sheria katika operesheni ya Nur Shams "na kwamba ISF ilitumia Wapalestina wasiokuwa na silaha kukinga vikosi vyao dhidi ya mashambulizi na kuwaua wengine katika hukumu ya wazi ya kunyongwa".

Makumi waliripotiwa kuzuiliwa na kutendewa vibaya huku ISF "ikisababisha uharibifu usio na kifani na wa dhahiri kwenye kambi na miundombinu yake", amedai Kamishna Mkuu.