Kujifungua kwa upasuaji kwakosesha mtoto fursa ya kunyonya maziwa ya mama punde tu anapozaliwa- WHO

Mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa amelala kwenye mikono ya mama yake katika kituo cha afya huko Accra, nchini Ghana
UNICEF/Giacomo Pirozzi
Mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa amelala kwenye mikono ya mama yake katika kituo cha afya huko Accra, nchini Ghana

Kujifungua kwa upasuaji kwakosesha mtoto fursa ya kunyonya maziwa ya mama punde tu anapozaliwa- WHO

Afya

Umoja wa Mataifa unasema kuwa bado watoto wanakumbwa na changamoto kubwa ya kunyonya maziwa ya mama zao pale tu wanapozaliwa. Hata kwenye hospitali zenye wataalamu wabobezi bado watoto wananyimwa haki yao hiyo ambayo ni muhimu ili kuchagiza makuzi yao.

Kuelekea kuanza kwa wiki ya unyonyeshaji duniani tarehe mosi mwezi ujao, shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema watoto 3 kati ya 5 wanakosa fursa ya kunyonya maziwa ya mama zao punde tu wanapozaliwa na hivyo kuwaweka hatarini kupata magonjwa na pia kufariki dunia. Siraj Kalyango na ripoti kamili.

Kilio cha mtoto mchanga hicho, kikiashiria heri baada ya mama yake kujifungua! Ni kwenye moja ya vituo vya afya nchini Nigeria. Wakunga wamempokea mtoto huyu taratibu za vipimo zinaendelea.

Kwa mtoto huyu na wengine wengi, mustakhbali wa uhai wao uko mashakani kwa kuwa wanakosa maziwa ya mama ndani ya kipindi cha saa moja tangu kuzaliwa.

Kupitia ripoti  yake iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi, WHO inasema watoto milioni 78 ulimwenguni kote hawapati maziwa ya mama punde wanapozaliwa.
 
Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni watoto kupatiwa vinywaji vingine kando mwa maziwa ya mama pamoja na ongezeko la uzazi kwa upasuaji.

Masita Lemorin mwenye umri wa miaka 26 akimyonyesha mwanae mwenye umri wa miezi 4 huko Port au Prince nchini Haiti
UNICEF/Marco Dormino
Masita Lemorin mwenye umri wa miaka 26 akimyonyesha mwanae mwenye umri wa miezi 4 huko Port au Prince nchini Haiti

Maaike Arts ni mtaalamu wa lishe kutoka shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na anaelezea athari za mtoto kukosa maziwa ya mama punde tu akizaliwa.

“Inasaidia kuanza kunyonyesha kwa usahihi, inazuia mtoto kufariki dunia miezi ya mwanzo ya uhai na pia inawakinga dhidi ya magonjwa," amesema Bi. Arts.

Awali UNICEF iliamini kuwa iwapo mjamzito atajifungua kwa msaada wa mkunga mwenye stadi basi mtoto lazima atanyonyeshwa hata hivyo, "kwa bahati mbaya, kuwe na mtaalamu, iwe hospitalini au kituo cha afya tunaona kuwa msaada huo haupo, wakati mwingine mtoto anapatiwa vimiminika au chakula kingine, au mtoto na mama wanatenganishwa, au hatua nyingine zisizo za lazima zinazuia kuanza kunyonyesha saa ya kwanza.”

Mama akimnyonyesha mwanae aliyezaliwa njiti kwenye kituo cha usaidizi wa wazazi huko Port au Prince nchini Haiti
UNICEF/Marco Dormino
Mama akimnyonyesha mwanae aliyezaliwa njiti kwenye kituo cha usaidizi wa wazazi huko Port au Prince nchini Haiti

Misri imetolewa mfano ambako asilimia 19 tu ya watoto wanaozaliwa kwa njia ya upasuaji ndio wanapata fursa ya kunyonya maziwa ikilinganishwa na asilimia 39 ya watoto wanaozaliwa kwa njia ya kawaida.
 
Huko jamhuri ya Dominika, kiwango cha wanaonyonyeshwa maziwa ya mama baada ya kuzaliwa kwa operesheni ni asilimia 40 ikilinganishwa na asilimia 61 ya wale wanaozaliwa kwa njia ya kawaida.
 
Hata hivyo ripoti inaweka bayana kuwa hata kujifungua kwa usaidizi wa mkunga mbobezi au kwenye kituo cha afya hakuongezi fursa ya mtoto kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, jambo linalothibitisha kuwa fursa hiyo sasa inakosekana kwa kila mtoto mchanga anayezaliwa.