Bado idadi kubwa ya watoto hawajawahi kunyonya maziwa ya mama: UNICEF
Idadi ya watoto wanaokosa kunyonya maziwa ya mama bado ni kubwa hususan miongoni mwa nchi tajiri duniani umesema uchambuzi mpya uliotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
Uchambuzi huo unasema takribani watoto milioni 7.6 kote duniani hawanyonyeshwi mazima ya mama kila mwaka. Maaike Arts ni mtaalamu wa masuala ya lishe wa UNICEF mjini New York amesema changamoto kubwa kwa wanawake ni msaada na será.
(SAUTI YA MAAIKE ARTS)
“Wanawake wanahitaji msaada ili kunyonyesha, ambao unajumuisha sera. Inamaanisha msaada kutoka kwa wahudumu wa afya, mila na desturi, jamii ambazo zinasaidia wanawake. Hivyo msaada huu hivi sasa haupatikani ipasavyo katika nchi za kipato cha juu ukilinganisha na zile nchi za kipato cha chini.”
Uchambuzi huo wa UNICEF unaonyesha kwamba ingawa unyonyeshaji wa maziwa ya mama unaokoa maisha, kulinda watoto na mama dhidi ya maradhi hatari na kuongeza ufahamu wa kiakili wa mtoto, inakadiriwa kwamba asilimia 21 ya watoto katika nchi tajiri hawajawahi kunyonyeshwa. Na katika nchi za kipato cha chini na wastani kiwango ni asilimia 4. Akisistiza umuhimu wa kunyonyesha Bi Arts amesema
(SAUTI YA MAAIKE ARTS-2)
“Tunachofahamu ni kwamba unyonyeshaji ni muhimu sana kwa watoto na kina mama pia. Kwa watoto unapunguza kiwango cha vifo vya mapema , unazuia idadi kubwa ya magonjwa kana kichomi na kuharisha, lakini pia fursa ya kuwa tipwatipwa. Na kwa kina mama tunaona kwamba unapunguza nafasi ya kupata saratani ya matiti, pia unalinda dhidi ya saratani ya mirija ya uzazi na kisukari.”
Ameongeza kuwa ili kuchagiza kina mama kunyonyesha hasa katika nchi tajiri, ni kuongeza ufadhili , sera za likizo ya uzazi, kuruhusu unyonyeshaji katika maeneo ya kazi, sera za kupunguza biashara ya maziwa mbadala, chupa na pia msaada unaohitajika pindi mama anapojifungua.
Baadhi ya nchi zilizo na kiwango cha juu cha unyonyeshaji watoto ni Bhutan,Madagascar na Peru zote zikiwa na asilimia 99, wakati nchi tajiri kama Irelani ni asilimi 55, na Marekani asilimia 74 , Marekani pia inashikilia theluthi moja kati ya watoto milioni 2.6 ambao hawajawahi kunyonyeshwa duniani.