Serikali ziwekeze zaidi ili watoto wanyonye maziwa ya mama zao wanapozaliwa-UN

1 Agosti 2018

Wiki ya unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama ikianza hii leo, Umoja wa Mataifa umesema utashi wa kisiasa ndio muarobaini wa kufanikisha suala la kuwezesha mtoto kunyonya maziwa ya mama yake punde tu anapozaliwa.

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF, Henrietta H. Fore na lile la afya WHO, Dkt. Tedros Gebreyesus wamesema hayo katika tahariri iliyotochapishwa kwenye tovuti  ya WHO.

Wamesema kupitia maadhimisho hayo ambayo ujumbe wake mwaka huu ni unyonyeshaji maziwa ya mama ni msingi wa uhai, serikali na wananchi wanatambua umuhimu wa kunyonyesha watoto maziwa ya mama.

Wametaja faida za maziwa ya mwanzo kabisa kutoka titi la mama baada ya kujifungua kuwa ni sawa na chanjo  ya kwanza kwa mtoto, inalinda mwili na inachochea kinga ya mwili.

“Katika siku za kwanza kabisa za mtoto, maziwa ya mama yanatofautisha  uhai na kifo,” wamesema viongozi hao wakiongeza kuwa iwapo unyonyeshaji huo utafanyika kwa usahihi, basi kila mwaka unaweza kuokoa uhai wa watoto 823,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Baba akiwa na mwanae pamoja na  mama wakati akinyonyesha  mtoto wake mchanga kwenye wodi ya wazazi nchini Armenia
UNICEF/Giacomo Pirozzi
Baba akiwa na mwanae pamoja na mama wakati akinyonyesha mtoto wake mchanga kwenye wodi ya wazazi nchini Armenia

Kutoka Tanga nchini Tanzania Sakina Mustapha ambay eni afisa lishe jijini humo anafafanua zaidi umuhimu wa maziwa hayo..

(Sauti ya Sakina Mustapha).

Kwa mujibu wa kadi ya ubia wa unyonyeshaji watoto duniani ukileta pamoja zaidi ya mashirika 20 ya kimataifa, uwekezaji zaidi unahitajika ili kuwezesha watoto kunyonya maziwa ya mama yao punde tu wakizaliwa.

Mathalani kuelekeza fedha kwenye mipango ya kufanikisha unyoyeshaji wa watoto, ufuatiliaji wa mifumo iliyopo, kuongeza likizo za uzazi kwa mama na baba na kuboresha vituo vya ushauri nasaha na usaidizi wa kunyonyesha watoto.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter