UNMISS yawanoa Polisi Sudan Kusini kuhusu ulinzi kwa watoto

26 Julai 2018

Maafisa 23 wa jeshi la polisi la Sudan Kusini wanaohudumu kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  humo cha UNMISS wamekutana  kwa ajili ya mafunzo maalumu ya kuwalinda watoto katika sehemu za migogoro.

Ni wakati wa kujitambulisha mjini Juba kwa maafisa hao walio na jukumu la kuwalinda watoto. Wametoka sehemu tofauti za Sudan Kusini kwalengo la kujifunza mbinu  bora za  kuwalinda watoto, kama anavyosisitiza kamishna wa polisi wa UNMISS, Bi. Unaisi Lutu Vuniwaqa.

(SAUTI YA UNAISI LUTU VUNIWAQA) 

“  Tunaona umuhimu   wa kuwamulika watoto, hususan waathirika wa makosa ya jinai, watoto kama mashahidi, na watoto kama washukiwa pia. Kuna haja kwetu kupigia debe uimarishaji wa mifumo ya sheria , hasa wakati  huu tunaposhirikiana na  wenzetu hapa polisi wa taifa la Sudan Kusini, kwamba tunahitaji kuendeleza  haki za watoto wanapokabiliana na sheria.”

Darasa limeanza, maafisa hao wa polisi wanajifunza kwa makini jinsi ya kutekeleza kwa vitendo,  elimu na  mbinu wanazopata .  Aja Ndey Begay Mbye ni mmoja wa maafisa hao

(SAUTI YA AJA NDEY BEGAY MBYE) 

“Najifunza jinsi ya kukabiliana na watoto, jinsi gani ya kuwahoji, jinsi ya kuwa nao na kuwaonyesha watoto hao mimi ni mama.”

 

Aja Ndey Mbye, Afisa wa UNPOL kutoka kikosi cha Gambia anacheza na watoto katika eneo la ulinzi wa raia nchini Sudan Kusini. Picha: UM/Video Capture
Aja Ndey Mbye, Afisa wa UNPOL kutoka kikosi cha Gambia anacheza na watoto katika eneo la ulinzi wa raia nchini Sudan Kusini. Picha: UM/Video Capture

Maafisa hawa  wametoka miji kama Juba,Wau,Bor, Bentui, Aweil, Rumbek, Torit pamoja na Yambio . Afisa polisi kutoka Uganda, Julius Ogwang,  anatoa taswira  ya kusikitisha  ya hali ya watoto anakofanyia kazi.

(SAUTI YA JULIUS OGWANG) 

 “ Hali ya kuwalinda watoto katika sehemu za Yambio hairidhishi kutokana na mgogoro unaoendelea  bila kikomo na pia kutokana na tatizo la UKIMWI na VVU. Unajua Yambio ndiyo inayoongoza majimbo yote nchini Sudan Kusini, kwa hivyo watoto wengi wamepoteza  wazazi  na hivyo wako hatarini.”

 

Polisi wa Umoja wa Mataifa akiwa na watoto. (Picha/UNPolice)
Polisi wa Umoja wa Mataifa akiwa na watoto. (Picha/UNPolice)

 

 Kamishina Vuniwaqa anasema baada ya mafunzo maafisa hawa watawafunza wengine katika maeneo yao kwa kuwapa mbinu muafaka za jinsi ya kujumuika na watoto.

(SAUTI YA UNAISI LUTU VUNIWAQA) 

 “Ni vema wakirudi katika majimbo yao wakaweza  kubadilishana ujuzi na polisi wengine wa Umoja wa Mataifa-UNPOL ili waweze kuyajumuisha mafunzo hayo katika kazi zao za kawaida za kila siku  pamoja na  mpango mzima wanaouendesha na polisi wa taifa wa Sudan Kusini.”

Pia amesema anaamini kuwa mafunzo haya yanafungua ukurasa mpya kwa ulinzi wa watoto Sudan  Kusini.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud