Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa afurahishwa na makubalino ya pande zinazokinzana nchini Sudan

Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya mji mkuu Khartoum Sudan Aprili 11, 2019
Ahmed Bahhar/Masarib
Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya mji mkuu Khartoum Sudan Aprili 11, 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa afurahishwa na makubalino ya pande zinazokinzana nchini Sudan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York Marekani, ameeleza kuhamasika na makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili zilizokuwa zinakinzana ikiwa ni hatua ya kuelekea katika kuundwa kwa serikali ya mpito.

Bwana Guterres ameupongeza Muungano wa Afrika na Ethiopia kwa ushiriki wao katika kusimamia mazungumzo yalioongozwa na wasudani na pia ameipongeza mamlaka ya kibiashara ya nchi za kaskazini mashariki, IGAD kwa kuusaidia mchakato mzima.

Aidha Bwana Guterres amehamasisha wadau wote kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa, yanatekelezwa kwa haraka, kwa kuhusisha pande zote na kwa uwazi na pia kutatua masuala yote ambayo hayajatatuliwa kwa njia ya majadiliano. Pia amekaribisha ahadi ya pande zote katika mgogoro, kufanya uchunguzi huru kuhusu vurugu zilizofanywa dhidi ya waliokuwa wanaandamana kwa amani, yakiwemo matukio yaliyotokea tarehe 3 ya mwezi Juni mwaka huu wa 2019.

Vilevile Guterres ameeleza kuwa yuko pamoja na watu wa Sudan na akarejelea ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia katika mchakato wa mpito wa kuelekea katika uundwaji wa serikali mpya.

Tangu Jeshi nchini humo lilipomuondoa madarakani rais Omar al-Bashir mwezi Aprili, maelfu ya watu wameendelea kuandamana kwenye miji mbalimbali ya Sudani kutaka mabadiliko ya utawala na kukabidhiwa kwa raia. Hata hivyo maanadamano hayo yamekuwa na makabiliano makubwa kati ya wananchi na wanajeshi kiasi cha watu kupoteza maisha na wengi kujeruhiwa. Mathalani jumapili tu ya wiki iliyopita, kulikuwa na maandamano ya nchi nzima ambapo karibani watu 7 waliripotiwa kupoteza maisha na zaidi ya watu 180 kujeruhiwa.

Awali mazungumzo kati ya baraza la mpito la kijeshi na upinzani yalivunjika baada ya tarehe 3 mwezi Juni hadi wakati huu makubaliano mapya yanayotazamiwa na wengi kuwa huenda yataleta muafaka yalipofikiwa hii leo tarehe 5 ya mwezi Julai 2019.