Heko Eritrea na Ethiopia kwa kujali uhusiano wenu- Guterres

21 Juni 2018

Ethiopia na Eritrea zimechukua hatua kusaka suluhu ya mambo yanayozua mtafaruku mara kwa mara kati yao.

Hatua hiyo imekaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York, Marekani.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa nchi mbili hizo zimekubali kuwa na mazungumzo ya amani, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1998 wakati vita mpakani mwa Eritrea na Ethiopia vilipoibuka na kusababisha kuuawa kwa makumi ya maelfu ya watu.

Guterres amesema uamuzi huo in hatua chanya ya kusuluhisha masuala yaliyosalia katika kuwezesha kurejesha uhusiano kati ya nchi mbili hizo.

Amepongeza jitihada za viongozi wa Eritrea na Ethiopia za kufikia amani endelevu na ujirani mwema akisema hatimaye zitakuwa na athari chanya kwenye eneo zima la pembe ya Afrika.

Katibu Mkuu amesema kwa upande wake  yupo tayari kutoa msaada wowote unaotakiwa ili kuchangia katika kusongesha na kuimarisha mchakato wa mazungumzo kati ya Ethiopia na Eritrea.

Tayari Rais Isaias Afwerki wa Eritrea amesema jana kuwa atatuma ujumbe wake kwenye nchi jirani ya Ethiopia kwa mazungumzo hayo.

Kauli ya Rais Afwerki inafuatia tangazo la mwezi uliopita la Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ya kwamba ataheshimu kikamilifu hadidu za rejea za makubaliano ya amani na Eritrea ya mwaka 2000, hatua ambayo ilitajwa ni ya kipekee.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter