Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CAR imeajiandaa vyema kukabili Ebola- WHO

WHO/S. Saporito — Sierra Leone.(MAKTABA)
Harakati za kuelimisha dhidi ya Ebola. Picha: WHO/S. Saporito — Sierra Leone.(MAKTABA)

CAR imeajiandaa vyema kukabili Ebola- WHO

Afya

Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR imeanza kazi ya kuhakikisha kuwa iko tayari kukabiliana na mlipuko wowote wa Ebola iwapo utaripotiwa nchini humo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo mwishoni mwa ziara yake nchini humo kwa kuzingatia kuwa CAR ni jirani na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ambako tayari Ebola imesababisha vifo.

Akiwa CAR, ameshuhudia kiwango cha maandalizi iwapo Ebola italipuka sambamba na hatua za ufuatiliaji na ukaguzi wa watu katika bandari ya mto Ouango Sao, eneo ambako linatumiwa na wasafiri wengi wanaoingia nchini humo.

Halikadhalika alikagua uwezo wa taasisi ya Bangui ambayo ina maabara ya kuchunguza sampuli na kuthibtishwa iwapo mshukiwa wa Ebola ana virusi vya ugonjwa huo au la.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema ingawa maandalizi yako vyema, mamlaka husika hazipaswi kubweteka bali kuimarisha jitihada hizo na kuepusha kabisa Ebola.

Wakati wa ziara hiyo Dkt. Ghebreyesus alikuwa na mazungumzo pia na Rais Faustin-Archange Touadéra, waziri wa afya na idadi ya watu Dkt. Pierre Somse na wadau wa masuala ya kibinadamu na mashirika ya kiraia.

CAR ni miongoni mwa nchi 9 ambazo WHO ilitangaza hivi karibuni itazijengea uwezo ili ziweze kukabiliana na Ebola iwapo ugonjwa huo utalipuka kwenye nchi hizo.