Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shida tunazo lakini tunahaha kulinda mitaa yetu- Vijana

Jayathma Wickramanayake (kushoto) mjumbe maalum wa UN kwa ajili  ya vijana akihutubia Baraza la Usalama wakati wa mkutano kuhusu vijana na amani na usalama duniani tarehe 23 Aprili 2018 jijini  New York, Marekani
UN /Mark Garten
Jayathma Wickramanayake (kushoto) mjumbe maalum wa UN kwa ajili ya vijana akihutubia Baraza la Usalama wakati wa mkutano kuhusu vijana na amani na usalama duniani tarehe 23 Aprili 2018 jijini New York, Marekani

Shida tunazo lakini tunahaha kulinda mitaa yetu- Vijana

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jayathma Wickramanayake kutoka Sri Lanka amesema sasa vijana siyo tena kundi la ziada kwenye masuala ya amani na usalama, bali ni kundi muhimu zaidi katika kufanikisha ajenda hiyo.

Akiwa ni mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa, kijana huyo wa kike amesema hoja hiyo ni dhahiri shahiri kwa kuzingatia kuwa Baraza la Usalama ambamo ndio ametolea kauli hiyo, limeitisha kikao cha kujadili vijana na amani na usalama duniani, kwa kuzingatia ripoti ya maoni kutoka vijana zaidi ya 4000 kote duniani.

Amesema vijana wamepitia mengi akikumbukia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake Sri Lanka ambako makazi yao yalikuwa ni kwenye mahandaki, milio ya risasi na milipuko ikichachamaa lakini ilimpa nia ya kwamba wakafi utafika atapata fursa achukue hatua, na sasa yametimia.

Image
Umoja wa kimataifa kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kuwaelimisha kuhusu malengo ya maendeleo endelevu SDG's. Picha: Photo - Zainul Mzige

Kwa mantiki hiyo Jayathma akawaambia wajumbe..

(Sauti ya Jayatma Wickramanayake)

Mosi, ungeni mkono kazi ya ujenzi wa amani zinazofanywa na vijana. Zitambueni, zipatieni fedha, ongezeni wigo wake na mzilinde. Vijana wengi wanafanya kazi za ulinzi wa amani mashinani lakini katu hazipatiwi kipaumbele. Pili patieni kipaumbele ushiriki wa vijana kwenye siasa ili washiriki kikamilifu. Hii ni pamoja na kwenye meza za mazungumzo kama vile Sudan Kusini, Yemen, Myanmar na kwingineko.”

Mjumbe akahitimisha hotuba yake kwa kupendekeza pia Baraza hilo lijenge ubia na vijana akisema mjadala wa wazi wa leo ni fursa ya kupanua wigo wa kuendeleza vijana wanaochangia katika ujenzi wa amani.

Kijana mwingine aliyehutubia kikao hicho ni  Sophia Pierre-Antoine kutoka Haiti ambaye ni miongoni mwa walioshiriki kwenye utafiti wa ripoti iliyowasilishwa kwenye baraza hilo.

Image
Vijana wachukua picha ya pamoja katika siku ya vijana Agosti mwaka huu. Picha: UM

Sophie amesema ingawa amezaliwa na kukulia katika mazingira hatarishi bado yeye na wenzake hawajakata tamaa.

(Sauti ya Sophia Pierre-Antoine)

“Sisi ndio ambao tunaongoza harakati za kila siku za kuhakisha usalama mitaani kwetu, amani nyumbani kwetu na haki kwenye jamii zetu.”

Sophia amesema wanatekeleza hayo wakiwa na msaada kidogo sana hivyo amesema.

(Sauti ya Sophia Pierre-Antoine)

“Ni kwa kusaidia mipango yetu na harakati zetu na kuimarisha ubia wetu na kuhakikisha ushiriki jumuishi ndipo amani endelevu itakuwa halisia.”