Mwaka 2017-2019
Mwaka 2017-2019
Mwaka 2017 ulianza kwa Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuanza rasmi hatamu yake ya uongozi na kuahidi kuleta mabadiliko katika usawa wa kijinsia na kuzuia mizozo katika dunia yenye migawanyiko.
“Tuko duniani iliyogawanyika, tunahitaji kuwa dunia iliyoungana.”
Janga kubwa lilishuhudiwa nchini Myanmar ambapo jamii ya warohingya laki sita walilazimika kukimbia makwao kuelekea Bangladesh ambako miundombinu imezidiwa uwezo.
Nchini Yemen watu milioni 8.5 wako katika hatari ya ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa.
Mwaka huu pia kulikuwa na shambulio baya dhidi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa kushuhudiwa kwa miongo kadhaa lililosababisha watu wengi zaidi kupoteza maisha ambapo walinda amani 14 kutoka Tanzania waliuwawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC. Balozi Modest Mero ni mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa wakati huo alisema
"Sisi kama watanzania tutaendelea kuendeleza amani kwa sababu uwezo tunao na nia tunayo , na pia na sehgemu ambayo sisi tumejitoa kimataifa kwamba tutalinda amani dunianani na hatuwezi kuwacha."
Takriban wahamiaji laki moja walivuka baharí ya Mediterranea kueleka Ulaya huku wahamiaji takriban 3,000 wakizama na kupoteza maisha wengi wakikimbia machafuko na hali mbaya ya kiuchumi kusini mwa jangwa la Sahara.
Mwaka 2018
Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Liberia UNMIL Machi 30 ulifunga rasmi milango baada ya kuhudumu kwa miaka 15
UNMIL uliweka mazingira mazuri kiusalama yaliyowawezesha zaidi ya wakimbizi milioni moja na watu waliofurushwa kurejea nyumbani, uliunga mkono chaguzi tatu za rais na kusaidia serikali kuunda mamlaka kote nchini kufuatia miaka ya mapigano na ukosefu wa usalama.
Mwaka 2018 Umoja wa Mataifa na kwingineko watu walikusanyika kumuaga aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan kufuatia kifo chake Agosti 18.
Mwaka 2019 Katibu Mkuu aliongoza mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambapo katika kikao hicho mwanaharakati kijana wa mazingira kutoka Sweden Greta Thunberg hakuficha hasira zake kutokana na hali ya sasa,
Anasema, “mmeiba ndoto zangu na utoto wangu kwa maneno matupu na mimi ni miongoni mwa walio na bahati, watu wanakabiliwa na madhila. Watu wanakufa. Mfumo wa ikolojia unakufa. Tuko katika mwanzo wa kutokomea, na kile ambacho mnaweza kuzungumzia ni maswala ya fedha na hadithi kuhusu ukuaji wa milele wa uchumi. Mnathubutu vipi?”
Kuelekea mwaka ujao Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 75 tangu kuasisiwa na ili kuadhimisha siku hiyo kutazinduliwa majadiliano ya 75 ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya sayari dunia tunayoitaka