Hakuna aliyezaliwa gaidi duniani ni mkanganyiko wa mambo:Guterres

17 Aprili 2018

Hakuna mtu aliyezaliwa gaidi na hakuna sababu yoyote inayohalalisha ugaidi. Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika mkutano wa 16 wa bodi ya ushari ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na ugaidi unaofanyika Saudia.

Guterres amesema inafahamika kwamba sababu mbalimbali zikiwemo migogoro ya muda mrefu isiyotatuliwa, kutokuwepo utawala wa sheria na sababu za kijamii na kiuchumi zinazotenga baadhi ya makundi vinaweza kuwa chahu ya kubadili machungu na mitazamo ya watu kuwa ya uharibifu kama ugaidi lakini si kitu cha kuzaliwa nacho.

Ameongeza kuwa wakati huu mashambulizi ya kigaidi yakiongezeka kila kona ya dunia na mengine yakisambaratisha kabisa jamii na hata kanda, mkutano huu ni fursa muhimu ya kuangalia jinsi gani kituo hicho ya kukabiliana na ugaidi kinaweza kuimarisha uwezo wake na msaada kwa nchi wachanama kupambana na uhalifu huo wa kimataifa.

Mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujadili vita dhidi ya ugaidi na usafiri wa anga. Picha: UM/Manuel Elias
Mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujadili vita dhidi ya ugaidi na usafiri wa anga. Picha: UM/Manuel Elias

Ametaja masuala matatu ya muhimu katika vita dhidi ya ugaidi , mosi amesema kunahitajika kuwa na mtazamo endelevu katika kuzuia ugaidi, ikiwemo hatua za kijeshi na kiusalama, pili  kituo hicho ni lazima kiendelee kukidhi mahitaji yanayobadilika ya nchi wanachama kwa msaada wa kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ugaidi na tatu kunahitajika kupanua wigo wa wahisani wa kituo hicho ili kuhakikisha ufadhili endelevu katika vita dhidi ya ugaidi.

Ameushukuru Ufalme wa Saudia kwa msaada mkubwa unaotoa kwa kituo hicho , na kuahidi kwamba mwezi juni atafanya mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa ukihusisha viongozi wa ngazi ya juu wa mashirika ya kupambana na ugaidi kutoka nchi wanachama , lengo likiwa kuimarisha ushirikiano katika ngazi zote za kikanda na kimataifa.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter