Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushughulikie madhila ya vijana ili kuepusha ugaidi- Guterres

Raia katika mji wa Mosul, Iraq baada ya shambulio la gari la  kujitoa mhanga.
UNHCR/Ivor Prickett
Raia katika mji wa Mosul, Iraq baada ya shambulio la gari la kujitoa mhanga.

Tushughulikie madhila ya vijana ili kuepusha ugaidi- Guterres

Amani na Usalama

Masuala ya wapiganaji mamluki, ushawishi wa vijana kutumbukia kwenye vitendo vya kigaidi na kitendo cha vijana hao kuona wameenguliwa kwenye masuala yanayowahusu yameangaziwa katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu kukabiliana na uagidi ulioanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Mkutano huo umeitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hotuba yake ya ufunguzi amesema hivi sasa magaidi wanatumia vibaya mitandao ya kijamii na mawasiliano yaliyowekewa ishara za siri kueneza propaganda chafu, kusaka wafuasi wapya na kuratibu mashambulizi.

Amesema ingawa vikundi vya ISIL vilishindwa kijeshi huko Iraq na Syria mwaka jana, hii inamaanisha wapiganaji mamluki wa kigaidi wanasaka maeneo mapya ya kuendeleza harakati zao..

“Wakati baadhi yao wanaweza kuwa wamekata tamaa na hawataki tena ghasia, wengine bado wameazimia kupeleka utalaamu wao kwenye uwanja wa mapigano kwa kusajili wafuasi wapya na kufanya mashambulizi. Magaidi wanaotokana na hali za nyumbani kwao nao wanaweka majaribuni uwezo wa mamlaka za kiusalama na kiintelijensia”

Na kama hiyo haitoshi amesema, magaidi nao hivi sasa wanalenga maeneo ambayo ni rahisi wao kutekeleza mashambulizi yao lakini ni vigumu kwa mamlaka kuweza kubaini na kuzuia mashambulizi.

Magari  yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.
UN /Stuart Price
Magari yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima kuwa na mikakati mtambuka akisema jambo muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja kwani ugaidi unaovuka mipaka nao unahitaji ushirikiano wa kimataifa kuudhibiti.

Katibu Mkuu amegusia pia vijana akisema wao ndio walengwa wakuu kwa hususan kwenye maeneo ambako wanahisi wamepuuzwa.

“Ni jambo la kusikitisha kuwa wasajiliwa wapya kwenye vikundi vya kigaidi  wana umri wa kati ya miaka 17 hadi 27. Vikundi vya kigaidi vinatumia ile dhana inayofanya vijana wa kike na wa kiume wajione wa kipekee, tofauti na maadili ya kijamii. Magaidi wanaangalia shida za vijana na ndio maana ni lazima tujitahidi kuzishughulikia.”

Na ni kwa mantiki  hiyo Katibu Mku ametaja malengo sita ambayo anataka washiriki wa mkutano huo wa siku mbili wayapatie kipaumbele.

Mosi ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kukabiliana na ugaidi akitaja mkakati wa kimataifa dhidi ya ugaidi uliopitishwa miaka 12 iliyopita. “Kuwa na mkakati pekee haitoshi bali tunahitaji utekelezaji upatiwe kipaumbele na utashi thabiti wa kisiasa na rasililimali za kutekeleza,” amesema Katibu Mkuu

Lengo la pili ni washiriki kurejelea na kuendeleza mtazamo wao katika kuzuia ugaidi akisema kuwa “tunahitaji kuondoka katika kukabiliana na tuelekee kwenye kuzuia, hii ina maana kuweka juhudi katika visababishi vya watu kuvutiwa na ugaidi.”

Tuondokane na kukabili ugaidi na badala yake tujikite zaidi kwenye kuzuia ugaidi na hiyo ndio njia bora zaidi.

Walinda amani wa UN kutoka CHad wakikagua mabomu ya kutegwa ardhini yanayotumiwa na vikundi vya kigaidi huko Mali.
UN /Sylvain Liechti
Walinda amani wa UN kutoka CHad wakikagua mabomu ya kutegwa ardhini yanayotumiwa na vikundi vya kigaidi huko Mali.

Vijana nao ni miongoni mwa malengo yake akisema ndio matumaini ya mustakhbali wa dunia na hivyo ni lazima kutumia vyema nguvukazi hiyo kwa kuwekeza kwenye elimu na fursa za ajira. Halikadhalika kuwapatia mbinu wanazohitaji kutokomeza dhana kandamizi za misimamo mikali.

Lengo la tano ni kwa washiriki kuangazia gharama ya kibinadamu itokanayo na ugaidi akisema Umoja wa Mataifa una wajibu wa kulinda haki za waliouwa na ugaidi, manusura wa ugaidi, na pia kusaka haki na kuhakikisha sauti zao zinasikika.

Kwa mantiki hiyo, “Nakaribisha uamuzi wa kuadhimisha kwa mara ya kwanza siku ya kimataifa ya kumbukizi ya wahanga wa ugaidi tarehe 21 mwezi Agosti.”

Na mwisho kabisa Katibu Mkuu amesema ni matumaini yake mkutano huo utaimarisha dhima ya Umoja wa Mataifa katika kusaidia wadau wote kukabiliana na ugaidi.

Hapo Kesho mkutano huo utaleta pamoja wawakilishi wa mashirika ya kiraia wanaofanya kazi kuelimisha umma huko mashinani kuhusu athari za ugaidi.