Ujasiri wa manusura wa ugaidi ni fundisho kwetu sote- UN

Baadhi ya washiriki wa kongamano la kupambana na ugaidi lililoandaliwa na shirika la waathirika wa ugaidi nchini Kenya, VITOK huko kaunti ya Kakamega nchini Kenya.
VITOK
Baadhi ya washiriki wa kongamano la kupambana na ugaidi lililoandaliwa na shirika la waathirika wa ugaidi nchini Kenya, VITOK huko kaunti ya Kakamega nchini Kenya.

Ujasiri wa manusura wa ugaidi ni fundisho kwetu sote- UN

Amani na Usalama

Leo ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kumbukizi na kutoa heshima kwa wahanga wa ugaidi  duniani, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni fursa ya kusikiliza sauti zao pamoja na waathirika wa vitendo hivyo kama njia ya kufanikisha vita dhidi ya ugaidi duniani.

Guerres katika ujumbe wake mahsusi kwa siku hii ambayo ni mara ya kwanza kabisa kuadhimishwa na Umoja wa Mataifa, amesema “sote tunaweza kujifunza kutokana na uzoefu wao. Jamii duniani kote zinaonyesha mnepo wao katika kukabiiliana na mashambulizi ya kigaidi. Zinapambana na ugaidi katika maisha yao ya kila siku, katika shule zao, masokoni na maeneo ya ibada.”

Hivyo amesema kusaidia makundi hayo ni jambo jema la kimaadili kwa kuzingatia wajibu wa kuendeleza, kulinda na kuheshimu haki zao za binadamu.

“Tunaposaidia waathirika na manusura wa ugaidi, kusikiliza sauti zao, kuheshimu haki zao na kuwapatia msaada na haki, tunakuwa tunaheshimu utangamano wetu na kupunguza kiwango cha madhara yanayofanywa na magaida kwa mtu mmoja mmoja, familia na jamii,” amesema Katibu Mkuu.

UN News/Patrick Newman

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, hatua za pamoja dhidi ya ugaidi ni muhimu kwa kuwa kitendo hicho ni moja ya changamoto kubwa zinazokabili ulimwengu hivi sasa na ni tishio kubwa la amani na usalama.

Amesema hakuna nchi iliyo salama, “kuanzia Tajikistan hadi Uingereza, kutoka Baghdad hadi Barcelona, mashambulizi haya ya kikatili yametutikisa sote kwa kiasi kikubwa na karibu kila taifa limekuwa muathirika wa ugaidi.”

Katibu Mkuu amesema hata Umoja wa Mataifa nao hulengwa akitolea mfano shambulio dhidi ya ofisi za chombo hicho huko Baghdad, Iraq mwaka 2003 ambako wafanyakazi 22 waliuawa.

Ametoa shukrani kwa manusura na waathirika wa ugaidia ambao wako tayari kuzungumza dhidi ya ugaidi akisema “sauti zenu ni muhimu, na ujasiri wenu katika mazingira magumu ni fundisho kwetu sote.Leo na kila siku Umoja wa Mataifa unashikamana nanyi.”

Kupitia azimio lake namba 72/165 la mwaka 2017, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha tarehe 21 mwezi Agosti iwe siku ya kumbukizi na kutoa heshima kwa wahanga wa ugaidi kwa lengo la kusaidia waathirika na manusura wa ugaidi, sambamba na kuendeleza na kulinda haki zao na uhuru wao wa msingi.