Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwa mkimbizi sio kukosa matumaini kwa wanawake wa Rohingya: UNHCR

Picha: UNICEF
Mama na mtoto wake mchanga, moja kati ya familia mpya za Rohingya ambao waliwasili Banglades mnamo tarehe 5 Septemba 2017.

Kuwa mkimbizi sio kukosa matumaini kwa wanawake wa Rohingya: UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Maelfu ya wanawake wa Rohingya waliokimbia machafuko nchini Myanmar na kupata hifadhi ya ukimbizi Bangladesh, sasa wameanza kuona nyota ya jaha baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kuwapa mafunzo ya ufundi cherahani. 

Kambini Nayapara Cox’s Bazar nchini Bangladesh katika moja ya karakana ya ushonaji, wanawake takriban 40 wakimbizi wa Rohingya wakipata mafunzo mapya na kujiunga katika mtandao mdogo unaokuwa kwa kasi katika taaluma ya ufundi cherahani ili kusaidia familia zao lakini pia kushika tena usukani wa maisha yao, asante UNHCR. Nasma Aktar ana umri wa miaka 19 ni mmoja wao

(SAUTI YA NASMA KATRA)

“Sikuwa najua kushona cherahani hapo kabla, nimejifunza baada ya kuja hapa, na kisha nikanunua cherahani na sasa naifanyia kazi na kupata fedha za kusaidia familia yangu.”

Kina mama hawa wanashona chupi na taulo za kike au pedi ambazo zinadumu kwa muda mrefu kwani zinaweza kufuliwa na kutumika tena na ni bidhaa muhimu sana kwa wanawake wakimbizi ambao asilimia kubwa ni wanawake na wasichana. Laila Arjuman Banu ni mchagizazi na fundi msaidizi katika karakana hiyo na anasema mafunzo haya yanawapa ujasiri mkubwa na

(SAUTI YA LAILA ARJUMAN BANU)

“Wanahisi fahari, kwani wanajifunza wenyewe na pia kuwasaidia wengine kujifunza.”
Lengo  la UNHCR ni kuwafunza wanawake wengine 1,200 mwaka huu ili kuwawesha kwani inaamini kuwa ukimbizi sio kupoteza matumaini.