Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yahaha kunusuru warohingya dhidi ya pepo za monsuni

Mvua kubwa zinatatiza ufikiaji wa maeneo ya mashinani katika kambi ya Cox’s Bazar
IOM 2018
Mvua kubwa zinatatiza ufikiaji wa maeneo ya mashinani katika kambi ya Cox’s Bazar

UN yahaha kunusuru warohingya dhidi ya pepo za monsuni

Wahamiaji na Wakimbizi

Pepo za monsuni huko barani Asia zimeanza kuonyesha uharibifu wake hususan kwa wakimbizi wa Rohingya walioko kwenye kambi ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh. 

Mvua hizo kubwa kama zilizovyokuwa zimetabiriwa zilianza jumamosi na kunyesha kwa siku mbili mfululizo kwenye kambi hizo zinazohifadhi wakimbizi wa Rohingya kutoka Myanmar.

Wahudumu wa kibinadamu wameripoti matukio 9 ya uharibifu ikiwemo maporomoko ya udongo, kutwama kwa maji, upepo m kali na radi.

Mratibu wa masuala ya dharura wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, Manuel Pereira akizungumzia kinachoendelea sasa amesema takribani watu milioni moja wanaishi kwenye miinuko, ambako udongo ni wa kifusi na hakuna miti wala vichaka kuepusha mmomonyoko.

Amesema wanachofanya sasa ni kurejesha miundombinu ikiwemo barabara na mitaro ya maji na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mvua, sambamba na kupatia wakimbizi huduma muhimu kama vile maji, vifaa vya kujisafi, ulinzi na makazi wakati huu wa mvua kubwa.

Hata hivyo amesema fedha zaidi zinahitajika ili kuendelea kutoa msaada wa kibinadamu wakati wa msimu huu wa mvua.

Bwana Pereira amesema kuwa bila msaada wanaweza kusitisha operesheni zao kwa kuwa wamepatiwa asilimia 22 tu ya fedha wanazohitaji na kuna hatari fedha hizo zitamalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu wa mvua, IOM na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa likiwemo lila la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la mpango wa chakula, WFP waliweka mtambo wa mashine kwa lengo la kusaidia mradi wa kurekebisha na kunyanyua ardhi kama njia mojawapo ya kupunguza mmomonyoko wa udongo.

Kupitia mpango huo waliandaa eneo la kuhamishia angalau watu 7,000.