Mitambo ya maji inayoendeshwa kwa nishati ya jua yaleta nuru kwa warohingya.

4 Januari 2019

Mifumo mitano ya  mitambo ya maji inayoendeshwa kwa nishati ya jua katika makazi ya wakimbizi warohingya huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh kwa sasa inafanya kazi kwa kiwango kinachostahili, ameeleza leo msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Andrej Mahecic mjini Geneva, Uswisi.

Bwana Mahecic ameongeza kuwa mifumo hii mipya inayosimamiwa na kuendeshwa na UNHCR, inaboresha usambazaji wa kila siku wa maji safi na salama ya kunywa kwa wakimbizi wa Rohingya wanaoishi katika mazingira yenye watu wengi kusini mashariki mwa Bangladesh.

“Mradi huo uliofadhiliwa na UNHCR ni moja ya mabadiliko makubwa katika utoaji wa misaada ya kibinadamu ambayo kwa kiasi kikubwa inatumia teknolojia isiyochafua hewa” ameeleza msemaji wa UNHCR.

Aidha ameongeza kuwa, mifumo hii mipya ya maji salama kwa kila namna inatumia umeme unaotokana na jua. Pampu zinachukua maji kutoka katika matanki yaliyotiwa dawa ya Chlorine yakiwa na lita 70,000 kisha maji hayo husukumwa hadi katika vituo vidogo vidogo katika makazi ya Kutupalong-Balukhali. UNHCR inalenga kumpatia kila mkimbizi lita 20 za maji safi na salama kila siku.

Zaidi ya wakimbizi warohingya 900,000 wanaishi katika maeneo mbalimbali ya eneo la Cox’s Bazar na kuna uhaba wa maji katika maeneo mengi. Wakati wa ukame mathalani, suluhisho pekee katika eneo la Nayapara huko nchini Bangladesh ni maji yanayoletwa kwa malori, na mfumo huo ni wa gharama kubwa.

Imekuwa ni changamoto kuwapatia maji wakimbizi wote, wengi wao wakiwa waameingia Bangladesh mwishoni mwaka 2017 ndiyo maana UNCR na wadau wake wakaingilia kati kujaribu kulitatua tatizo hiloamesema Mahecic

Matumizi ya nishati ya jua yamesaidia mashirika ya kuhudumia wakimbizi kupunguza gharama za nishati na pia uchafuzi wa hewa. Uwekaji wa dawa ya Chlorine pia kumeonesha ni mwokozi wa maisha kwa wakimbizi kwani vipimo vya hivi karibuni vimeonesha kuwa maji yalikuwa yanachafuka wakati wa kuyakusanya, kuyasafirisha na kuyatunza majumbani.

UNHCR inasema maji yaliyowekewa dawa hiyo ni salama kwa kunywa na yanaondoa hatari ya kusambaza magonjwa. Vyanzo vya maji vya awali hususani mabwawa ambayo yalikuwa na pampu za kusukumwa kwa mkono yalikuwa yanachafuka kutokana na maji taka ambayo yanapenya katika mabwawa.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter