Ulinzi na usalama Ghouta bado mtihani mkubwa:Moumtzis

4 Machi 2018

Mtaratibu wa kikanda wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya mgogoro wa Syria amesema anaendelea kutiwa hofu ya usalama na ulinzi wa mamilioni ya raia nchini Syria, ikiwa ni wiki moja tangu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lipige kura kuunga mkono azimio  nambari 2401, linalotaka usitishaji wa mapigano kwa mwezi mmoja nchini Syria.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Panos Moumtzis, amesema sio kwamba hatua hiyo haijafanyika, bali pi katika sehemu zingine ghasia zimeongezeka hususani kwa raia 400,000 wanaume, wanawake na watoto Mashariki mwa Ghouta.

Ameongeza kuwa badala ya afueni kubwa iliyotarajiwa sasa mapigano zaidi yanashuhudiwa, vifo zaidi, habari zaidi za kusikitisha za njaa na hospitali kushambuliwa kwa mabomu na kusema adhabu hii ya pamoja dhidi ya raia haikubaliki.

Karibu watu 400,000 wanaishi katika eneo linalozingirwa la Ghouta Mashariki, ikiwa ni asilimi 94 ya jumla ya watu wote wanaoishi maeneo yanayozingirwa nchini Syria.
UNHCR/Assadullah Amin
Karibu watu 400,000 wanaishi katika eneo linalozingirwa la Ghouta Mashariki, ikiwa ni asilimi 94 ya jumla ya watu wote wanaoishi maeneo yanayozingirwa nchini Syria.

 

Tangu tarehe 18 Februari takriban watu 600 wamearifiwa kuuawa katika mashambulizi ya anga kwenye eneo hilo lililozingirwa huku wengine zaidi ya 2000 wakijeruhiwa.

Wakati huohuo mashambulizi na makombora yanayovurumishwa kutokea ardhini Mashariki mwa Ghouta yamekatili na kujeruhi raia kwenye mji wa jirani wa Damascus.

Umoja wa Mataifa na mashirika wadau wa misaada ya kibinadamu wako tayari kuwasaidia watu milioni 13.1 ndani ya Syria lakini hawawezi kufanya hivyo peke yao na hususani mapigano yakiendelea, hivyo Moumtzis ametoa wito kwa pande zote katika mzozo kuheshimu azimio la baraza la usalama na sheria za kimataifa za kibinadamu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter