Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twasema yatosha, dunia yataka tuendelee kupigwa- Wakazi Ghouta

Ru'a mwenye umri wa miezi 18, akiwa juu ya baiskeli ya babu yake wakati wakivuka eneo la Mesraba huko Ghouta Mashariki nchini Syria
UNICEF/2018/Amer Almohibany
Ru'a mwenye umri wa miezi 18, akiwa juu ya baiskeli ya babu yake wakati wakivuka eneo la Mesraba huko Ghouta Mashariki nchini Syria

Twasema yatosha, dunia yataka tuendelee kupigwa- Wakazi Ghouta

Amani na Usalama

Kwa mara nyingine tena jamii ya kimataifa inaendelea kulaumiwa na wakazi wa Ghouta Mashariki kwa kutochukua hatua kukomesha ukatili unaoendelea kwenye eneo hilo nchini Syria. Makombora yanatesa raia na sasa sauti zao kutoka uwanja wa mapigano zimewasilishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mapigano huko Ghouta Mashariki nchini Syria yakiendelea kugharimu maisha ya watu, hii leo wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamepatiwa nukuu za mashuhuda ya athari za makombora yanayoendelea kuporomoshwa kwenye eneo hilo kwa mfululizo tangu tarehe 4 mwezi huu.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa  Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, Mark Lowcock amesoma nukuu hizo zilizowasilishwa kwao na wafanyakazi wa kutoa misaada nchini Syria.

Katika nukuu hii Bwana Lowcock anasema kuna familia nzima inalengwa. Mama na watoto wake watatu. Wanawake wajawazito wanne.

Anaendelea na nukuu akisema mjamzito mmoja amefariki dunia, mmoja yuko mahututi, mwingine wa tatu amepoteza mtoto wake, wa nne anafanyiwa uchunguzi..

Mtoto akiwa amebeba mfuko wenye kuni huko Ghouta Mashariki nchini Syria.
UNICEF/Al Shami
Mtoto akiwa amebeba mfuko wenye kuni huko Ghouta Mashariki nchini Syria.

​​​​​​​Mtoto wa kike amepoteza macho yake yote na mashambulizi  yanaendelea..

Je mnasikia sauti zetu? Hali inakuwa ya kutisha. Mahandaki yetu si salama tena! Tusaidieni! Kuweni nasi jamani! Badala ya kusema inatosha, dunia inasema ongeza tena!

Hivyo Bwana Lowcock akageukia wajumbe wa Baraza la Usalama na kusema..

(Sauti ya Mark Lowcock)

“Bado mnaweza kuokoa maisha huko Ghouta Mashariki na kwingineko nchini Syria. Nawasihi mfanye hivyo. Mamilioni ya watoto, wanawame na wanaume walioshambuliwa na kukumbwa na ukatili wanategemea hatua kutoka baraza hili.”

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein wamepazia sauti ghasia na ukatili unaoendelea Ghouta Mashariki.