Skip to main content

Dola bilioni 7 zaahidiwa kwenye mkutano wa mshikamano na Syria:UN

Mtoto mkimbizi wa Syria akiwa nje ya hema kwenye kambi yao nchini Lebanon
UNICEF/Alessio Romenzi
Mtoto mkimbizi wa Syria akiwa nje ya hema kwenye kambi yao nchini Lebanon

Dola bilioni 7 zaahidiwa kwenye mkutano wa mshikamano na Syria:UN

Msaada wa Kibinadamu

Wahisani wa kimataifa leo wameahidi dola bilioni bilioni 6.97  mjini Brussels Ubelgiji katika mkutano wa mshikamano na watu wa Syria ili kusaidia mamilioni ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu nchini Syria  lakini pia wakimbizi, na jamii zinazowahifadhi katika nchi jirani.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA sehemu ya fedha za ahadi hizo , bilioni 2.5 ni kwa ajili ya mwaka huu kupelekwa kwenye kituo cha Muungangano wa Ulaya kwa ajili ya wakimbizi kilichopo Uturuki .

Mwaka 2017 wahisani waliahidi dola bilioni 6 mjini Brusells na mwaka 2018 ahadi ilikuwa n idola bilioni 4.4 na hadi kufikia mwisho wa mwaka jana jumla ya dola bilioni 6 zilichangishwa.

Awali katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa ujumbe kwa njia ya video akisema baada ya miaka nane ya vita nchini Syria madhila kwa mamilioni ya watu bado yako palepale na hali haijatengamaa  .

Katika ujumbe wake maalumu kwenye mkutano wa mshikamano kwa ajili ya mstakabali wa Syria na ukanda mzima unaofanyika mjini Brussel nchini Ubelgiji tangu Machi 12 Guterres amesema zaidi ya watu milioni 11 ndani ya Syria wanahitaji msaada wa kibinadamu na wengi wao wanakabiliwa na ukatili  wa kila aina kila siku.

Ameongeza kuwa: watu wengine milioni 5.6 wakiimbia nchi hiyo na kwenda nchi jirani bila kufahamu lini wataweza kurejea nyumbani kwa usalama na utu.” Hivi sasa Umoja wa Mataifa na mashirika wadau wanatoa msaada wa kuokoa maisha ikiwemo chakula, maji safi, huduma za afya na msaada wa ulinzi kwa mamilioni ya watu kila mwezi na hili linawezekana tu kwa sababu ya ukarimu wenu wa kutoa msaada na kwa asanteni sana kwa kuendelea na mshikamano.”

Pia amewataka wahisani hao kuongeza ahadi zao za kifedha, misaada ya kibinadamu na kisiasa kwa watu wa Syria, nchi na jamii zinazowahifadhi wakimbizi.

Amesisitiza kuwa suluhu pekee ya mzozo wa Syria ni ya kisiasa kwa kuzingatia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2254.

Wakimbizi wakiwa kambi ya Al-Hol katika jimbo la Hasakeh kasakzini mashariki mwa Syria.
UNICEF/UN037295/Soulaiman
Wakimbizi wakiwa kambi ya Al-Hol katika jimbo la Hasakeh kasakzini mashariki mwa Syria.

 

Hali inazidi kuwa tete katika baadhi ya maeneo-Lowcock

Mkuu wa masuala wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA , Mark Lowcock amesema hali inazidi kurozota na kutisha nchini Syria hususan katika eneo la Idlin Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo ambako zaidi ya watu 90 wameuawa kutokana na makombora na mashambulizi ya anga mwezi uliopita na karibu nusu ya watu hao ni watoto. Akiuuelezea mgogoro wa Syria kama moja ya zahma kubwa katika kizazi hili amesema “kiwango kikubwa cha mashambulizi ya kijeshi Idlib kitazusha zahma mbaya zaidi ya kibinadamu ambayo dunia haijawahi kuishuhudia katika karne hii ya 21.”

Kwingineko Syria amesema hali imetulia kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita ingawa ameonya kwamba “mseneo ya mwisho yanayodhibitiwa na ISIL Kaskazini Mashariki kunashuhudiwa machafuko yanayoendelea na mabaya zaidi. Na mbali ya vitisho vya usalama kutokna na vita Wasyria wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha ambapo watu 8 kati ya 10 wanaishi chini ya mstari wa umasikini na gharama za chakula zimeongezeka mara sita zaidi ya ilivyokuwa kabla ya vita. Ametaka ahadi za fedha na misaada mingine viongezwe ili kunusuru maisha ya mamilioni ya watu walio wakimbizi wa ndani na nje ambao maisha yao hayatakuwepo bila misaada ya kibinadamu.

Mwanamke akiwa akiwa amesimama katika nyumba yake katika viunga vya El Khalideh, mjini Homs Syria. (Machi 2019)
UNHCR/Andrew McConnell
Mwanamke akiwa akiwa amesimama katika nyumba yake katika viunga vya El Khalideh, mjini Homs Syria. (Machi 2019)

 

Mambo matatu ya kuzingatia tunapoisaidia Syria-Grandi

Naye Kamishina Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa Filippo Grandi aliyehitimisha ziara yake wiki iliyopita mjini Damascus, Homs na Hama amesema ameguswa sana na mnepo wa hali ya juu walionao watu wa Syria ambao licha ya vita vya kutwa kucha na madhila ya hali ya juu wanayoyapitia , wamejizatiti kujenga upya maisha yao na jamii zao.

Ameongeza kuwa “Kukiwa bado na uharibifu mkubwa , ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo na ukosefu wa huduma za msingi kama chakula, madawa, ajira na maji safi, Wasyria wengi wanarejea nyumbani.”

Amesisitiza kuwa wahudumu wa misaada wa kimataifa na mashirika mengine wanafanya kila wawezalo , lakini bado hali ni mbaya kutokana na ongezeko kubwa la wakimbizi wa ndani na wakimbizi wengine kuamua kurejea nyumbani hali ilizozidisha mahitaji.

Grandi amesema kama kuna ujumbe ambao ni lazima utoke kwenye mkutano huu ni kwamba ukarimu w anchi zinazowahifadhi uchukuliwe kwa uzito wa juu. Amesema anaafiki hoja kwamba suluhu kwa ajili ya wasyria inahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote na kwamantiki hiyo ameainisha maombi matatu ambayo “Mosi ongezeko la misaada lililo na uhakika kupelekwa kwa nchi za jirani zinazowahifadhi watu wkutoka Syria, pili  tunahitaji aeneo zaidi ya kuwapa makazi ya kudumu wakimbizi na tatu ni kuwajumuisha wakimbizi na wakimbizi wa ndani katika maandalizi ya kuwarejesha nyumbani.

Dola bilioni 5.5 zinahitajika mwaka huu 2019 ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 9.4 wakiwemo wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.

Na baada ya kukunjwa jamvi la mkutano huo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA limesema historia imefanyika baada ya kutolewa ahadi ya  dola bilioni 7 kama sehemu ya zaidi ya dola bilioni 8 zinazohitajika kwa ajili ya kikidhi mahitaji ya Wasyria walioko ndani ya nchi, wakimbizi wa ndani , wakimbizi walioko nje na jamii zinazowahifadhi.