Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Askari watoto 300 watoka katika makundi ya waasi Sudan Kusini

Picha hii ya maktaba inaonyesha askari watoto walioachiliwa huru Sudan Kusini
UNICEF/2015/South Sudan/Sebastian Rich
Picha hii ya maktaba inaonyesha askari watoto walioachiliwa huru Sudan Kusini

Askari watoto 300 watoka katika makundi ya waasi Sudan Kusini

Amani na Usalama

Zaidi ya askari watoto 300 waliokuwa wapiganaji wakiwemo wasichana 87 leo, wameachiliwa huru na makundi kadhaa ya wapiganaji  nchini Sudan Kusini. 

Hii ni ishara ya mwanzo wa mchakato wa kuona takriban watoto 700 kuweza kuachiliwa huru katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Akizungumzia tukio hilo la kwanza kufanywa na wapiganaji wenye silaha nchini humo kwa Zaidi ya mwaka mmoja,  mjumbe wa UNICEF, Mahimbo Mdoe, amesema hii ni hatua moja muhimu ya kufikia lengo kuu la kuhakikisha watoto wote ambao baado wanatumiwa kama askari wanaunganishwa tena na familia zao. Amesema idadi ya leo ya watoto 300 ndiyo kubwa kuwahi kufanywa katika kipindi cha miaka mitatu na ni muhimu kwa mazungumzo  kuendelea ili matukio kama hayo yaendelee kushuhudiwa.

Ameongeza kuwa watoto 215 waliachiliwa na kundi la South Sudan National Liberation Movement-SSNLM- ambalo mwaka 2016 lilitia saini mkataba wa amani na serikali na sasa linajumuishwa katika jeshi la serikali.

 Watoto wengine 96 wameachiliwa na kundi la South Sudan Peoples Liberation Army-In Opposition-SPLA-IO.

Mapigano ya Julai 2016 yalikwamisha zoezi la kuwaachilia watoto hao, lakini hatua hii ambayo imekaribishwa pia na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS bwana David Shearer imeelezwa kuleta matumaini

UNICEF, imesema mwaka huu 2018, inataka msaada  wa dola milioni 45 kuweza kufadhili mpango huo kikamilifu.