Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa watambua rasmi ufugaji nyuki

Mfugaji wa nyuki huko Lekit, Azerbaijan. Picha: FAO

Umoja wa Mataifa watambua rasmi ufugaji nyuki

Hatimaye ufugaji nyuki duniani umepigiwa chepuo baada ya Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuwa kila mwaka kuanzia tarehe 20 mwezi mei mwakani itakuwa ni siku ya ufugaji nyuki ulimwenguni. Selina Jerobon na ripoti kamili.

(Taarifa ya Selina)

Hatua hiyo imepongezwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva ambaye amesema uwepo wa siku hiyo unatoa fursa ya kuangazia zaidi kazi hiyo ambayo inachangia katika kutokomeza njaa pamoja na umaskini.

Amesema nyuki pamoja na viumbe vingine vinavyochavusha maua kama vile vipepeo, popo na ndege husaidia mimea ikiwemo ile ya chakula kuzalisha mazao.

Ametolea mfano nyuki mchavushaji ambaye kazi yake siyo tu kutembelea takribani maua 7,000 na kusaidia yachavue, bali pia hutengeneza asali ambayo inatumika kama chakula na pia kama dawa.

Bwana da Silva amesema ufugaji nyuki hivi sasa ni mkombozi kwa kuwa kinachotajika ni kiwango kidogo cha mtaji pamoja na eneo dogo la ardhi.

Umoja wa Mataifa umetenga siku hiyo ya mei 20 kwa kuzingatia kuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Anton Janša, ambaye wakati wa karne ya 18 alibuni mbinu za kisasa za ufugaji nyuki huko nchini mwake Solvenia.