UNICEF na WHO kutoa chanjo dhidi ya surua huko Bangladesh

10 Novemba 2017

Ongezeko la hofu ya kuwepo kwa wagonjwa wa surura miongoni mwa wakimbizi wapya wa Rohingya waliowasili hivi karibuni nchini Bangladesh, imesababisha mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya, WHO pamoja na serikali ya Bangladesh kuimarisha jitihada za chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwenye kambi   za wakimbizi.

UNICEF imesema karibu watoto 360 000 wenye  umri kati ya  miezi sita hadi miaka 15 kwenye eneo la Cox’s Bazar nchini Bangladesh watapatiwa chanjo na pia katika mipaka yote ya kuingia Bangladesh.

Bwana Edouard Beigbede ambaye ni mwakilishi wa UNICEF Bangladesh amesema tangu tarehe 4 mwezi huu tayari mtu moja amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa surua na wengine 412 wanashukiwa kuwa na ugonjwa huo hatari kwenye makazi ya muda na huko Cox’s Bazar.

Asilimia 82 ya walioathirika ni watoto chini wenye umri chini ya miaka mitano.

UNICEF imesema tayari warohingya 611,000 wamevuka mpaka kutoka Myanmar na kuingia Bangladesh tangu Agosti mwishoni na wanaishi katika hali duni.