Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna umuhimu wa kubadili mifumo ya mlo Asia Pasifiki- FAO

Kuna umuhimu wa kubadili mifumo ya mlo Asia Pasifiki- FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO leo limesema hatua za haraka za kuimarisha lishe na kubadili mifumo ya mlo ni muhimu kwa ajili ya kuwa na chakula bora na chenye afya katika eneo la Asia Pasifiki.

Kwa mujibu wa ripoti ya FAO ya mwaka 2017 kuhusu mtazamo wa kikanda juu ya uhakika wa chakula na lishe, kuna umuhimu wa kukabiliana na utapiamlo na kuhimiza ulaji wa lishe bora na kumaliza ulaji wa vyakula visivyo bora.

Kando na uwekezaji katika kilimo, ripoti imetaja umuhimmu wa  kuimarisha uwekezaji katika masuala mengine ili kukabiliana na utapiamlo kama vile huduma ya kujisafi, upatikanaji wa maji safi na salama, kuimarisha lishe ya watoto kwa siku elfu moja za mwanzo za uhai wao na sera za kuongeza ulaji wa vyakula vyenye virutubisho.

Wakati uhakika wa chakula umeimarika kwa mamilioni ya watu katika ukanda wa Asia Pasifiki, bado njaa na utapiamlo vimeongezeka katika baadhi ya maeneo huku ripoti ikionyesha kwamba takriban nusu bilioni ya watu hawapati chakula bora.

FAO imetaja watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuwa katika hali mbaya huku mmoja kati ya wanne amedumaa.

Hata hivyo utipwatipwa umeongezeka katika kipindi cha miaka 15 iliyopita hususan Asia Kusini.