Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen itatumbukia kwenye janga la njaa kama vizuizi haviondolewi

Yemen itatumbukia kwenye janga la njaa kama vizuizi haviondolewi

Mkuu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa, OCHA Mark Lowcock, amesema iwapo vizingiti vilivyowekwa nchini Yemen havitaondolewa, nchi hiyo sasa inatumbukia kwenye janga la njaa.

Amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhutubia kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Bwana Lowcock amesema ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia umeweka vizingiti vya usafiri vya hali ya juu akisema..

(Sauti ya Lowcock)

“Kama mjuavyo, hatua kadhaa zimeanzishwa hivi karibuni na ushirika huo ikiwemo kuzuia matumizi ya anga, bahari na barabara kwa ajili ya safari za kuingia Yemen. Nimelieleza Baraza kuwa iwapo vikwazo hivyo havitaondolewa na hatua tano nitakazozitaja hazitachukuliwa, Yemen itashuhudia janga la njaa. Haitakuwa njaa kama Sudan Kusini mwaka huu au Somalia mwaka 2011, la hasha!. Itakuwa ni janga la njaa ambalo halijawahi kushuhudia duniani na mamilioni ya watu waathirika.”

Bwana Lowcock ametaja hatua tano mahsusi ambazo anapendekeza ili kuepusha janga la njaa Yemen kuwa ni.

(Sauti ya Lowcock)

 “Mosi kurejesha mara moja huduma za usafiri wa anga za Umoja wa Mataifa na wadau wake wa misaada ya kibinadamu kwenye miji ya Sanaa and Aden. Pili iwekwe bayana kabisa katu hakutakuwepo na usitishaji wa safari za anga. Tatu makubaliano ya haraka ya eneo jipya la kutia nanga kwa meli za WFP kwenye pwani ya Aden na hakikisho kwamba hakutakuwa na usumbufu tena. “

Bwana Lowcock ametaja hatua ya nne kuwa ni kurejeshwa haraka kwa huduma za meli za biashara kwenye bandari Aden ili kusafirisha chakula, mafuta na dawa, na tano ni kuondoa vizuizi kwa misafara ya meli ambazo tayari zina kibali cha Umoja wa Mataifa ili ziweze kutia nanga haraka kwenye bandari ya Yemen.