Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Doria zaendelea CAR kusimamia amani

Doria zaendelea CAR kusimamia amani

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA wanaendelea na doria za mchana na usiku hasa kwenye mji mkuu, Bangui.

Ghasia zimeendelea kuibuka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kutishia mchakato wa amani ambao umewezesha kuundwa kwa serikali.

Makundi yaliyojihami ambayo yamegawanyika kwa misingi ya makabila na dini yamekuwa yakifanya mashambulizi lakini MINUSCA inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuna amani.

Zaidi ya raia milioni moja wa CAR wametapakaa maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kukimbia makwao tangu mzozo uanze nchini humo mwaka 2012.

Tayari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeomba askari wa ziada 900 ili kusaidia operesheni za MINUSCA.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kesho ataanza ziara nchini CAR ambapo ataangalia utendaji wa chombo anachoongoza na pia hali ya  kibinadamu.