Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani vikali shambulio la kigaidi Moghadishu:

UM walaani vikali shambulio la kigaidi Moghadishu:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea jana Jumamosi mjini Moghadishu nchini Somalia.

Kupitia taarifa ya msemaji wake iliyotolewa leo Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi.

Pia Katibu Mkuu aewapongeza wahudumu wa afya na wakazi wa Moghadishu ambao wamejitoa kimasomaso kusaidia wahanga wa shambulio hilo . Ameitaka Somalia kuungana katika vita dhidi ya ugaidi na itikadi kali na kufanya kazi pamoja kujenga serikali thabiti ya umoja wa Kitaifa.

image
Mwakilishi maalumu wa UM nchini Somalia na Mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM Michael Keating. Picha na UM
Naye mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini humo Michael Keating ameungana na jumuiya ya kimataifa katikia kulaani shambulio hilo lililokatili maisha ya watu zaidi ya 200 na kujeruhi wengine zaidi ya 200.

Amesema ni shambulio la kikatili lisilokubalika kwa aina yeyote ile na kipaumbele kwa sasa ni kutoa msaada unaohitajika kwa kushirikiana na serikali ya Somalia ili kuwasaidia wote walioathirika, hususani majeruhi na walioachwa bila makazi.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya kimataifa kwa ujumla watafanya kila liwezekanalo kuwasaidia watu na serikali ya Somalia kuikabili zahma hii.