Badilisha mwelekeo wa uhamiaji, wekeza vijijini- FAO

16 Oktoba 2017

Leo ni siku ya chakula duniani ambapo Umoja wa Mataifa unataka dunia iwekeze katika uhakika wa chakula na maendeleo ya vijijini ili kubadili mwelekeo wa uhamiaji utokanao na mabadiliko ya tabia nchi.

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linasema ingawa hivi sasa kuna hama hama kubwa zaidi ya binadamu kuwahi kutokea tangu vita kuu ya pili ya dunia ikihusishwa na mizozo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, athari za mabadiliko ya tabianchi nazo hazipaswi kusahauliwa.

FAO inasema sambamba na hilo, idadi kubwa ya watu wanaohamia ugenini wanasababisha changamoto ya chakula kwa kuwa rasilimali nazo ugenini ni finyu.

Kwa mantiki hiyo FAO inasema kuweka mazingira bora kwa wakazi wa vijijini hususan vijana ni muhimu ili wawe na shughuli za kujipatia kipato na hivyo kutohamia mijini au nchi nyingine.

Mathalani kuweka fursa za biashara na ajira kwa vijana, fursa zisizoegemea zaidi mazao ya kilimo kama vile ufugaji wa kuku na wanyama pamoja na matunda na mbogamboga.

Kwa kufanya hivyo, FAO inasema kutakuwa na uhakika wa upatikanaji siyo tu wa chakula bali pia kipato na pia kupunguza mgongano wa rasilimali.

FAO inaadhimisha tukio hilo kwa kufanyika mkutano wa ngazi ya mawaziri kwenye makao makuu ya shirika hilo huko Roma, Italia, tukio litakalohudhuriwa pia na kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis.