Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafanikio ya MINUSTAH Haiti kuendelezwa- Honoré

Mafanikio ya MINUSTAH Haiti kuendelezwa- Honoré

Mafanikio  yaliyopatikana nchini Haiti kutokana na uwepo wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSTAH yataendelea kuimarishwa na kuendelezwa wakati huu ambapo chombo hicho kinahitimisha shughuli zake na kuzikabidhi kwa ujumbe mdogo zaidi, MINUJUSTH.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Sandra Honoré amesema hayo leo jijini New York, Marekani wakati akihutubia Baraza la Usalama kwa mara ya mwisho kama mkuu wa MINUSTAH inayofunga rasmi kazi zake Jumapili hii.

Ametaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 13 cha uwepo wao kuwa ni pamoja na kukamilika kwa mchakato wa kisiasa uliowezesha kupatikana kwa Rais wa nchi na wawakilishi sambamba na kuundwa kwa taasisi za serikali, bunge  na mahakama.

(Sauti ya Sandra)

“Hakuna shaka: Mafanikio hayo na mengine ambayo sijayasema, ingawa ni muhimu bado ni hatua za awali. Jitihada za kina zitahitajika siyo kwa mamlaka za Haiti pekee, bali pia wadau wote ili kuimarisha mafanikio haya na kuhakikisha kuna utulivu wa kisiasa na kuendeleza utendaji wa taasisi za kidemokrasia na kuimarisha utoaji wa huduma zake kwa maslahi ya raia wa Haiti bila kusahau usaidizi wa marafiki wa kimataifa na wadau.”

Awali akihojiwa na Idhaa yaUmoja wa Mataifa aligusia ugonjwa Kipindupindu ambao Umoja wa Mataifa ulikiri kutochukua hatua muafaka na za kutosha kudhibiti na hivyo kuleta janga kwa wananchi wa Haiti akisema..

(Sauti ya Sandra)

 “Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia Haiti kutokomeza kipindupindu utaendelea hata baada ya MINUSTAH kuondoka nchini humo. Usaidizi huu haukutolewa kupitia MINUSTAH pekee bali pia kupitia mashirika mengine kama UNICEF na lile la afya kwa Amerika ya Kusini, PAHO. Na mwezi Juni mwaka huu Katibu Mkuu aliteua mjumbe wake maalum kwa Haiti na moja ya majukumu yake ni kuchangisha rasimali zinazotahitajika kutekeleza mkakati huo mpya.”

MINUJUSTH ambayo itaanza kazi rasmi tarehe 15 mwezi huu itakuwa ni  ujumbe mdogo zaidi  ukijitika katika usaidizi kwa serikali ya Haiti kwenye kuimarisha  utawala wa kisheria na ufuatiliaji wa haki za binadamu.