Uchaguzi DRC Hakuna kurudi nyuma na tusiingiliwe- Kabila

23 Septemba 2017

Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC itatangaza siku chache zijazo ratiba ya uchaguzi mkuu nchini humo kufuatia mashauriano ya utatu yaliyofanyika baina ya mamlaka ya kitaifa ya ufuatiliaji wa makubaliano ya uchaguzi, serikali na tume ya taifa ya uchaguzi.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amesema hayo hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la umoja huo.

Amesema hadi sasa watu milioni 42 wamejiandikisha kupiga kura kati ya milioni 45 wanaotarajiwa, huku uandikishaji ukifanyika hivi sasa katika majimbo mawili ya kati nchini humo.

Hata hivyo amesema…

(Sauti ya Kabila)

“Licha ya maendeleo haya, bado kuna changamoto kubwa katika maandalizi ya uchaguzi nchini mwangu ikiwemo  vifaa, usalama na fedha. Tunakabiliana na changamoto hizi  kwa unyenyekevu lakini na uthabiti pia. Kwa kuzingatia hatua tulizofikia, tuna uhakika wa kufanya chaguzi za haki, halali huru na wa amani. Hili ni jambo ambalo haliwezi kurudi nyuma na linapaswa kufanyika bila kuingiliwa na pande zozote za kigeni. Kwa rafiki zetu wa kweli, tunasihi mtupatie msaada wa dhati katika mchakato wetu wa uchaguzi.”

image
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. (Picha:UNWEBTV Video capture)

Hotuba yake pia imegusia masuala ya amani na usalama hususan maeneo ya kati ya Kasai ambako amesema vikundi vya kikabila vyenye silaha vinatumia raia hususan watoto kama silaha ya vita.Amesema ingawa idadi kubwa ya washukiwa wa matukio hayo wamekamatwa na mchakato wa mahakama za wazi unafanyika, lengo pi ni kusaka maridhiano baina ya jamii tofauti na ndio lengo la  mkutano wa amani, maridhiano na maendeleo ambao..

(Sauti ya Kabila)

“Lengo lake ni kusaka ukweli na mazingira ya kile kilichotokea kwenye majimbo ya kati ya nchi, na pia  kuendeleza maridhiano baina ya jamii za majimbo hayo. Nasisitiza kwamba kila maridhiano lazima yahusishe haki. Hakuna amani  ya kweli bila haki.”

Kuhusu mustakhbali wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ambao umekuwepo nchini humo kwa miaka 20 sasa, Rais Kabila amezungumzia tathmini ya kimkakati inayoendelea kati ya nchi yake na Umoja wa Mataifa akisema…

(Sauti ya Kabila)

“Tathmini hii ya kimkakati inapaswa kubainisha kasi ambayo kwayo jeshi la MONUSCO litapunguzwa hadi litakapoondoka kabisa. Ni dhahiri kuwa miaka 20 tangu ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuwasili nchini mwangu, hauwezi kusaka kuendelea kuwepo siku zote, au kuendelea kufanya kazi bila kujifunza na makosa yaliyobainishwa. Hii ni muhimu ili kupata kuwepo na uhalali wa chombo hicho na pia kukubalika. Ndio maana kwa miaka kadhaa sasa tunataka tathmini ya vikosi vya MONUSCO.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter