Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu kujadili utamaduni wa amani #CultureOfPeace

Baraza Kuu kujadili utamaduni wa amani #CultureOfPeace

Hii leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na kikao cha ngazi ya juu kikiangazia utamaduni wa amani, jambo ambalo linaelezwa kuwa hivi sasa linafifia.

Rais wa baraza hilo Peter Thomson amesema wakati wa kikao hicho wajumbe kwa kuzingatia mada hiyo watajadili jinsi ya kupanda mbegu ya utamaduni wa amani tangu utotoni.

Amesema kwa hali ilivyo sasa na mwelekeo wa kutekeleza lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu kuhusu haki na jamii jumuishi, utamaduni wa amani unasalia ndio nguzo kuu.

Mwenyekiti wa kikao hicho cha ngazi ya juu Balozi Anwarul K. Chowdhury amesema mbegu ya amani iko kwa kila mtu lakini ni lazima ipaliliwe kwa kuwa amani haiwezi kujengwa toka nje bali inapatikana kuanzia ndani ya mtu mwenyewe.

Miongoni mwa wazungumzaji ni mshauri mwandamizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu sera Ana Maria Menendez na mshindi wa tuzo ya Nobel Dkt. Betty Williams.