Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dhoruba Harvey limeleta hali ya jinamizi jimboni Texas-WMO

Dhoruba Harvey limeleta hali ya jinamizi jimboni Texas-WMO

Dhoruba inayokumba jimbo la Texas nchini Marekani ni jinamizi ambalo linaendelea, limesema shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO. Joseph Msami na ripoti kamili.

(Taarifa ya Joseph)

Hofu ikiendelea kutanda huko Texas, baada ya mvua kubwa na upepo mkali kukumba eneo hilo na kusababisha vifo na mafuriko, WMO imetoa onyo ikisema kuwa kimbunga Harvey kilichoanza kupiga Ijumaa iliyopita sasa kimebadilika na kuwa dhoruba.

WMO imesema mvua kubwa inayoandamana na kimbunga hicho Harvey imesababisha mafuriko katika maeneo ya Galveston na Houston huku ripoti zikisema kwamba watu watano wamefariki dunia.

Clare Nullis ni msemaji wa WMO

‘Utabiri wa hali ya hewa tulionao kwa sasa ni kwamba kimbunga hicho kinatarajiwa kusonga na kuelekea katika maeneo ya kati na juu ya pwani ya Texas na kupunguza kasi kuelekea Tennessee, kwa hiyo kasi ya upepo itapungua lakini kiwango cha mvua huenda kikasalia na hii ni mbaya. Kando na hatari itokanayo na upepo na maji, kimbunga ni hatari ambayo watu wanakabiliana nayo kama nilivyosema ni hali ya jinamizi.’

Mvua zinatarajiwa kufikia kiwango cha mita 1.2 huku WMO ikiongeza kwamba imelazimika kubuni majedwali mpya ya utabiri kwa sababu ya mvua nyingi.