Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafugaji walioghubikwa na ukame Ethiopia wahitaji msaada:FAO

Wafugaji walioghubikwa na ukame Ethiopia wahitaji msaada:FAO

Kusaidia wafugaji kurejea katika Maisha ya kawaida na kuzuia kupoteza zaidi mifugo yao ni muhimu sana nchini Ethipia kulikoghubikwa na ukame na njaa imekuwa ikiongezeka mwaka huu, limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO.

Ukame nchini Ethiopia umewaathiri vibaya wafugaji na Maisha yao, wakikosa malisho na maji na kusababisha idadi kubwa ya mifugo kufa au kuugua hususan katika eneo la Kusini na kusini Mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa FAO athari zingine kwa wafugaji hao ni upungufu wa uzalishaji wa maziwa, ongezeko la utapia mlo na kipato duni kilichochangia adha katika uwezo wa upatikanaji wa chakula.

Watu milioni 8.3 au mtu mmoja kati ya 12 anakabiliwa na njaa nchini humo na milioni 3.3 kati yao wanaishi katika jimbo la Somali.

FAO inasema kati ya sasa na Desemba inahitaji dola milioni 20 kuwasaidia wafugaji hao wakati msimu wa mvua unaanza ili waanze mchakato wa kurejea katika Maisha ya kawaida na kuzuia hasara zaidi.