Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Al-Shabaab yakatili maisha ya askari 12 wa Uganda Somalia

Al-Shabaab yakatili maisha ya askari 12 wa Uganda Somalia

Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating, leo ametuma salamu za rambirambi kwa wafanyakazi na familia za askari kutoka Uganda wa kulinda amani wa muungano wa Afrika nchini Somalia AMISOM waliouawa katika shambulio kwenye jimbo la Lower Shabelle jana jumapili.

Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na shambulio hilo lililokatili maisha ya askari 12 na kujeruhi wengine saba walipokuwa wakifanya doria ya pamoja na askari wa jeshi la Somalia. Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi la Uganda iliyotolewa mapema leo uchunguzi umeanzisha ili kubaini mazingira yaliyosababisha tukio hilo.

Keating amesema ‘tunawaenzi wanajeshi wa AMISOM ambao wamejitoa sadaka kwa ajili ya mustakhbali bora na wa amani Somalia”. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendeleza mashikamano na watu na serikali ya Uganda wakati huu wakiomboleza msiba mkubwa wa mashujaa wao. Pia amewatakia afueni ya haraka askari waliojeruhiwa katika shambulio hilo.