Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 420 zahitajika kunusuru hali mbaya katika pwani za Libya

Dola milioni 420 zahitajika kunusuru hali mbaya katika pwani za Libya

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema leo kuwa juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na maafa makubwa yanayotokana na safari za wakimbizi na wahamiaji katika pwani za Libya.

Mjumbe Maalum wa UNHCR kuhusu hali kwenye Mediterenia ya Kati, Vincent Cochetel amewaambia waandishi wa habari jjini Geneva, Uswisi kwamba, watu 2,360 wamepoteza maisha yao baharini katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, na idadi ya watu isiyojulikana pia wameangamia ndani ya nchi, ikiaminiwa kuwa ni waathirika wa biashara haramu na utekaji nyara.

Amesema UNHCR imesikia hadithi za kutisha za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa safari za watu kuja na kuondoka Libya, ukiukwaji huo ikiwa ni pamoja na kazi nzito za kulazimishwa kwa wale wasioweza kulipa gharama ya safari nzima mpaka pale walanguzi wanaporidhika, huku idadi kubwa ya wanawake wanafungwa ndani ya maghala na kulazimishwa kufanya ukahaba.

Libya kwa muda mrefu imekuwa ni kituo cha kazi kwa wahamiaji na wasaka hifadhi kutoka Niger na Algeria.

Bwana Cochetel amesema onyo la hatari ya safari hizo kwa wale wanaowasili Libya ni hatua nzuri, lakini kampeni ya mawasiliano pekee haitoshi kusitisha hali hii mbaya, na ndio maana shirika lake limetoa ombi la dola milioni 421 zitakazosaidia nchi jirani kuharakisha madai ya wasaka hifadhi pamoja na kuboresha huduma za mapokezi kwa wale wanaohitaji ulinzi.

Vile vile amesema angependa kuona kuwa Jumuiya ya Kimataifa inachukua hatua zaidi kupambana na makundi ya wahalifu ambao wanadhibiti mtiririko wa watu wanaovuka bahari ya Mediterenia.