Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja baada ya #WHS kuna mafanikio- O’Brien

Mwaka mmoja baada ya #WHS kuna mafanikio- O’Brien

Mwaka mmoja tangu kufanyika mkutano wa kimataifa wa utu wa kibinadamu, Umoja wa Mataifa umesema tukio hilo limeleta mabadiliko makubwa hasa katika mshikamano wa kusaidia watu milioni 135 wanaohitaji misaada ya kibinadamu hivi sasa.

Mkuu wa ofisi ya usaidizi wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa. OCHA,  Stephen O’Brien amesema kwa sasa kuna uratibu wa kutekeleza ajenda ya kibinadamu ikishirikisha wadau wote ukiwemo Umoja wa Mataifa, sekta binafsi na mashirika ya kiraia akisema…

(Sauti ya O’Brien)

“Siyo tu kushughulikia janga tukiwafikia bali pia kuanza kujenga upya maisha ambapo ni miradi ya kujikwamua na kuchipuka yaani ishi na chipuka.”

Akifafanua mpango huo amesema..

(Sauti ya O’Brien)

“Tuna miradi ya pamoja, tuna ufadhili wa pamoja na hii inaleta tofauti kubwa. Ni changamoto kubwa ukilinganisha na jinsi tulifanya kazi hapo awali. Lakini ni njia mpya ya kufanya kazi ambayo tunaamini italeta manufaa makubwa”

Mkuu huyo wa OCHA amesema hivi sasa kati ya watu milioni 135 wanaotegemea misaada ya kibinadamu dunian, milioni 93 wanahitaji misaada ya dharura.

image
Ahadi ambazo zilitangazwa wakati wa mkutano huo. (Picha:UN/WHS/Trelloboard)