Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za afya duniani kutamalaki wiki hii Geneva-WHO

Changamoto za afya duniani kutamalaki wiki hii Geneva-WHO

Jinsi ya kukabiliana na hatari kubwa kabisa za kiafya kwa binadamu ni suala lambalo linatamalaki kwenye baraza la 70 la afya ulimwenguni lililofungua pazia Jumatatu kwenye makao makuu ya shirika la afya duniani WHO mjini Geneva Uswis. Flora Nducha na taarifa kamili.

(TAARIFA YA FLORA)

Katika baraza hilo nchi wanachama wa WHO 194 wataketi na kujadili yapi waliyojifunza kutakana na milipuko ya karibuni ya maradhi kama Zika na Ebola.

Nao watalaamu kwa upande wao watatoa taarifa mpya za vipi mfano Angola iliweza kukabiliana na mlipuko wa homa ya manjano .

Masuala mengine yatakayotupia jicho ni pamoja na mlipuko wa kipindupindu unaoendelea Yemen, Polio huko Afghanistan, Pakistan na Nigeria. Akizungumza katika ufunguzi wa baraza hilo mkurugenzi mkuu wa WHO Dr Margaret Chan amesema

(SAUTI YA DR CHAN)

“Kunapozuka mlipuko , WHO inahitaji uzoefu wa kina kwa ajili ya kuwezesha kupatikana kwa dawa mpya, lakini uratibu duni unapoteza sana muda na ili kuharakisha mambo WHO na washirika wake wametoa muongozo mwaka 2016 utakaosaidia kupunguza muda wa kutengezeza dawa kutoka miaka hadi miezi”.

Jumla ya wawakilishi kutoka karibu nchi 200 wanashiriki baraza hilo ambapo Jumanne mchana pia watapiga kura kumchagua mkuu pya wa WHO kutoka kwa wagombea watatu Tedros Ghebreyesus kutoka Ethiopia, David Nabarro kutoka Uingereza na Sania Nishtar kutoka Pakistan na yeyote atakayeshina atakuwa mrithi wa Dr Margaret Chan,anayeachia ngazi baada ya kuhudumu kwa miaka 10.