Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wahamiaji na wakimbizi waliokwama Ulaya waathirika kisaikolojia na kijamii- UNICEF

Watoto wahamiaji na wakimbizi waliokwama Ulaya waathirika kisaikolojia na kijamii- UNICEF

Karibu wakimbizi na wahamiaji 75,000, wakiwemo watoto 24,600 waliokwama katika kambi za muda nchini Ugiriki, Bulgaria, Hungary na Magharibi mwa Balkans wako katika hatari ya kuathirika kisaikolojia na kijamii kunakosababishwa na kuishi katika hali ya sintofahamu kwa muda mrefu. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace)

Onyo hilo limetolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF likiongeza kuwa licha ya kuwa na haki ya kuungana na familia zao zilizopo Ulaya Mashariki, kama Ujerumani au Sweden, waomba hifadhi wengi hawajui endapo wataruhusiwa au lini wanaweza kufanya hivyo.

Hali ni mbaya zaidi hasa kwa wanawake wasio na waume na watoto ambao wamekwama Ugiriki na maeneo ya Balkans wakisubiri kuungana na familia zao zilizo katika nchi zingine za Ulaya.

Monie Al Sabsabi ni mama mkimbizi kutoka Aleppo, Syria

(SAUTI YA MONIE)

"Maisha ni magumu sana kambini, watoto hawajui waishije hapa, hakuna utulivu. Wameunda shule lakini hakuna mustakhali wa watoto hawa. Watoto wangu wanapoteza maisha yao ya baadaye, nami naumia kwa niaba yao, maisha yao yamesismama.”

UNICEF inasema idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaokwama Ugiriki, Hungary na Magharibi mwa Balkans imeongezeka kwa karibu asilimia 60 kutoka 47,000 Machi 2016 hadi kufikia 80,000 mwishoni mwa Aprili mwaka huu.