Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 25 hawasomi kwenye maeneo ya vita-UNICEF

Watoto milioni 25 hawasomi kwenye maeneo ya vita-UNICEF

Watoto zaidi ya milioni 25 wa kati ya umri wa miaka 6 na 15 , au asilimia 22 ya watoto wa umri huo hawasomi kwenye maeneo yenye mizozo katika nchi 22 dunianI, limesema Ijumaa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Amina Hassan ana taarifa kamili.

(Sauti ya Amina)

Hakuna wakati ulio muhimu sana kwa elimu kama wakati wa vita, imesema UNICEF ikihoji kwamba bila elimu ni jinsi gani watoto hao wataweza kuchangia katika mustakhbali na utulivu wa familia zao, jamii zao na uchumi wa nchi zao?.

Muzoon Almellehan, msichana mkimbizi wa Syria, mwanaharakati na mwakilishi wa UNICEF aliezuru Chad hivi karibuni anasema elimu inamaanisha nini haswa....

(Sauti ya Muzoon)

"Elimu ni kitu ambacho kinatupa kila kitu, inatupa nguvu, inatupa fursa na inatufungulia milango mingi mbele yetu, kwa njia ya elimu tunaweza kufikia matumaini na ndoto zetu, na pia tunaweza kuendeleza nchi zetu, kwa hiyo tukiwa na elimu, tunakuwa na nguvu".

Katika kiwango cha elimu ya msingi Sudan Kusini imetajwa kuongoza kwa kuwa na karibu asilimia 72 ya watoto ambao hawasomi, ikifuatiwa na Chad asilimia 50 na Afghanistan asilimia 46. Nchi hizo tatu pia ndizo zenye kiwango cha juu cha watoto wakike wasio na elimu.