Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliotawanywa na machafuko Mosoul wakaribia 500,000:OCHA

Waliotawanywa na machafuko Mosoul wakaribia 500,000:OCHA

Karibu watu nusu milioni wametawanywa tangu kuanza kwa operesheni ya kukomboa mji wa Mosoul Iraq kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la ISIL miezi sita iliyopita . Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Lise Grande ametoa taarifa Jumatatu akielezea idadi ya watu wanaokimbia mji huo wa Kaskazini mwa nchi kama ni kubwa mno.

Amesema mapigano yalipoanza Umoja wa Mataifa ulikadiria hali mbaya na kuwa hadi watu milioni moja watakimbia Mosoul. Hadi sasa zaidi ya watu 490,000 wameuhama mji huo. Wakati huohuo Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba hadi watu 500,000 wamesalia kwenye maeneo yanayodhibitiwa na ISIL Magharibi mwa Mosoul, wengi wakiwa katika mji wa kale ulio na watu wengi.

Watoa huduma za kibinadamu wameongeza wigo wa makazi ya dharura ili kuhifadhi melfu zaidi ya watu ambao huenda wakakimbia katika wiki chache zijazo.