UNICEF yapongeza sheria ya Zampa nchini Italia

UNICEF yapongeza sheria ya Zampa nchini Italia

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema sheria ya Zampa iliyopitishwa nchini Italia ni ya kihistoria katika ulinzi wa watoto wahamiaji na wakimbizi.

Watoto hao ni wale wanaokuwa wanasafiri wenyewe kuelekea Ulaya kusaka hifadhi ambapo UNICEF imesema ni ya kuigwa barani humo.

Mathalani sheria hiyo inataka kuwepo kwa msururu wa mikakati ikiwemo muda ambao watoto hao wanasubiri katika vituo vya mapokezi.

Halikadhalika inapigia chepuo huduma ya malezi na familia za wenyeji zinazoweza kuwachukua na kuwatunza.

Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi ya asilimia 90 ya watoto hao ambao huwa kwenye harakati za kutembea kusaka hifadhi kupitia bahari ya Mediteranea huwa wanasafiri peke yao.