Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukaji wa haki za binadamu DRC umeongezeka asilimia 30: UM

Ukiukaji wa haki za binadamu DRC umeongezeka asilimia 30: UM

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Andrew Gilmour ameesema ukiukaji wa haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa mwaka jana uliongezeka kwa asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Bwana Gilmour meyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu kinachoendelea huko Geneva, Uswis akiongeza kuwa ukiukwaji huo ni kuhusiana na kuzuia demokrasia na kuanza tena kwa shughuli za makundi kadhaa yenye silaha.

Ofisi yake imekosoa hatua ya matumizi ya nguvu kwa waandamanaji wakati wa mikutano ya hadhara au maandamano na yanayotekelezwa na vikosi vya usalama. Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu imetoa wito kwa mamlaka kupitisha kwa haraka sheria kuhusu uhuru wakuandamana kwa amani na sheria kuhusu watetezi wa haki za binadamu. Amesema ofisi yake piaimekuwa na wasiwasi kuhusu vurugu katika kile Serikali inachokiita "kanda zisizo na migogoro." Mauaji, majeraha, uharibifu wa mali na ukiukwaji mwingine katika mikoa ya Kasai na Lomani kwenye eneo la Kamuina Nsapu ambayo ni tishio kubwa kwa amani nchini.

Bwana Gilmour amekaribisha sera dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia iliotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na jitihada za kupunguza msongamano katika magereza. Amesema kuwa ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu iko tayari kusaidia uchunguzi wa serikali kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Maman Sambo Sidikou ambaye pia ni mkuu wa MOUNUSCO amesema wanahitajika rasilimali ili kuimarisha uwezo wao. Naye waziri wa haki za binadamu wa DR Congo Marie Ange Mushobekwa amelaani mauaji yaliyofanyika kwenye eneo hilo la Kasai na kuahidi msaada akisema kuwa watafanya kazi na MONUSCO katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mchakato wa utulivu.

Pia ameahidi kushirikiana na Umoja wa Afrikakuhakikisha wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo yote ya nchi watafikishwa mbele ya haki, wanafunguliwa mashitaka na kuhukumiwa akiongeza kuwa serikali ina nia ya kukuza na kulinda haki za binadamu ikishirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na kupunguza ukatili wa kijinsia ambapo kila mtu anawajibika, ikiwa ni pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi.