Skip to main content

UNHCR yalaani kushambuliwa kwa meli huko Yemen

UNHCR yalaani kushambuliwa kwa meli huko Yemen

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeshutumu kitendo cha kushambuliwa kwa meli moja iliyokuwa imebeba watu takribani 145 karibu na pwani ya Hudaydah nchini Yemen.

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo la Alhamisi lilisababisha vifo vya watu 42, miongoni mwao wakimbizi wanawake na watoto.

Amemnukuu Kamishna Mkuu wa UNHCR Filipo Grandi akitoa wito kwa pande husika kuwajibisha wahusika na kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena.

(Sauti ya Farhan)

“Wakati mazingira yaliyosababisha tukio hilo la Alhamisi bado hayako bayana, kwa mujibu wa sheria za kimataifa raia hawapaswi kushambuliwa na pande kinzani lazima zichukue kila hatua kulinda raia. Kwa sasa wafanyakazi wa UNHCR huko Yemen wamekuwa wakiwapatia misaada familia za waathirika na wahanga wa shambulio hilo.”