Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuepusha zahma Sudan Kusini msaada lazima ufike sasa: O'Brien

Kuepusha zahma Sudan Kusini msaada lazima ufike sasa: O'Brien

Mamia kwa maelfu ya watu nchini Sudan Kusini wataathirika zaidi na baa la njaa endapo wafanyakazi wa misaada hawatapata fursa ya kuwafikishia msaada waathirika na fedha zaidi za ufadhili kutolewa ameonya hii leo mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien.

Amesema hayo baada ya kusafiri hadi eneo la Ganyiel, jimbo la Unity,  moja ya maeneo yenye vurugu na kukutana na watoto walio kwenye hali mbaya ya utapiamlo.

Akiandika katika ukurasa wake kwenye tovuti ,O'Brien amesema hali inatishia, pia akiweka picha kadha za watu ambao wamekimbia mapigano na unyanyasaji wa kijinsia.

Tayari mashirika wa kibinadamu likiwemo la Kimataifa la Msalaba Mwekundu wameanzisha kliniki katika maeneo athirika ili kuwafikia watu wengi zaidi.

O'Brien ameongeza kuwa mamilioni ya watu wanazuiwa kupokea misaada na pande kinzani katika mgogoro na hii ni kinyume cha maadili, kinyume cha sheria na ni hali isiyokubalika.

Amesema kuwa usaidizi lazima upatikane sasa hivi. Mratibu huyo yuko nchini Sudan Kusini ili kujionea hali ya kibinadamu na ni nini shirika lake linaweza kufanya.