Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Soko la nyumba halizingatii haki za binadamu:UM

Soko la nyumba halizingatii haki za binadamu:UM

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya nyumba, Leilani Farha,  ameonya juu ya ukuaji wa soko la nyumba za kibiashara bila kujali haki za binadamu, halikadhalika ongezeko la gharama zake kiasi cha watu wengi kutomudu.

Akitoa ripoti yake ya hivi karibuni kwa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, mMtaalam huyo amesema, nyumba zimepoteza thamani ya kijamii na kubadilishwa kuwa  karibu chombo cha kujitajirisha, ikiwa imenyang’anywa kabisa heshima yake na maana ya nyumbani.

Amesema serikali nyingi zimeshabikia masoko ya kifedha  kwa njia inayosababisha watu wengi kutoweza kuzifikia, zikitupilia mbali wajibu wa kimataifa wa kulinda haki za biandamu zikisaka tu uwajibikaji kwa masoko na wawekezaji.

Farha amezitaka serikali kudhibiti wawekezaji binafsi katika sekta hiyo, sio tu kwa kuzuia ukiukwaji wa uwazi wa haki za binadamu, bali pia kutekeleza wajibu wa kuhakikisha haki ya nyumba kwa wote, iliyomulikwa katika ajenda 2030.