Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika itaendelea kuwa kipaumbele cha UM- Naibu Katibu Mkuu

Afrika itaendelea kuwa kipaumbele cha UM- Naibu Katibu Mkuu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed leo ameapishwa rasmi na Katibu Mkuu wa umoja huo António Guterres ili kushika wadhifa huo baada ya kuteuliwa mwishoni mwa mwaka jana.

Hafla ilifanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo baada ya kumwapisha naibu wake, Katibu Mkuu Guterres akafunguka..

(Sauti ya Guterres)

“Nina furaha ya kupindukia kuwa umejiunga nasi na ninajivunia sana kwamba umekubali kujiunga na timu yetu. Asante sana!”

Baada ya kuapishwa alifungua kwa niaba ya Katibu Mkuu, mkutano wa siku tatu wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, linalokutana kujadili shughuli zake za kiutendaji kwa miaka minne ijayo ambapo Bi. Mohammed amesema kuna nuru njema ya kimaendeleo..

image
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed katika mkutano wa siku tatu wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOCPicha: UN Photo/Eskinder Debebe
(Sauti ya Amina)

“Nimeshuhudia hili kwenye kanda zote, ikiwemo Afrika ambako nimeshuhudia umaskini ukipungua, fursa za kidemokrasia zikipanuka na watu wengi zaidi wakiunganishwa na teknolojia za mawasiliano. Hata hivyo kutokana na mazingira yake bado Afrika itaendelea kuwa kipaumbele cha Umoja wa Mataifa. Na kwa pande zote, mafanikio ya Afrika ni mafanikio ya dunia.”

Alipata fursa pia ya kuzungumza na waandishi wa habari ambapo aliulizwa nini mtazamo wake kuhusu ombi la Umoja wa Mataifa la dola bilioni nne kusaidia nchi nne zilizokumbwa na njaa zaidi barani Afrika.

image
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed akihutubia waandishi wa habari. Picha: UN Photo/Eskinder Debebe
(Sauti ya Amina)

“Tunashinikiza usaidizi tunaohitaji kwa nchi hizo nne, hii njaa haitajikita kwao tu iwapo hatutashughulikia suala hilo kidharura.”