Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya utawala wa Gaddafi haikuwa na viwango vya kimataifa

Kesi ya utawala wa Gaddafi haikuwa na viwango vya kimataifa

Kesi ya wajumbe wa utawala wa zamani wa Libya chini ya Muammar Gaddafi haikuwa na viwango vya kimataifa na ilipoteza fursa ya kutenda haki amesema Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa. Rosemary Musumba na taarifa kamili

(TAARIFA YA ROSE)

Zeid Ra'ad Al Hussein ametoa kauli hiyo kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu mwenendo wa kesi dhidi ya wawakilishi 37 wa serikali iliyomalizika mwaka 2015.

Watu hao walikamatwa baada ya machafuko ya mwaka 2011 ya kumpinga rais Gaddafi.

Tisa kati yao walihukumiwa kifo akiwemo mtoto wa Rais Gaddafi Saif al-Islam Gaddafi, ambaye hukumu yake ilisomwa bila yeye kuwepo. Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ukweli ni kwamba upande wa mashitaka haukuwasilisha ushahidi ushahidi mahakamani licha ya kwamba upo mwingi ulioandikwa.

Claudia Cordone anawakilisha ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Libya.

( Sauti Claudia)

‘‘Suala moja muhimu ni ukweli kwamba upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi mahakamani isipokuwa tu katika mtindo wa muhtasari mara moja pekee. Licha ya kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa maandishi uliofikishwa kwenye mahakama na kwa wanasheria lakini haukuwasilishwa mahakamani.’’

Katika ripoti hiyo ofisi ya haki za binadamu na mpango wa Umoja wa mataifa nchini Libya UNSMIL wamekaribisha juhudi za kuwajibisha maafisa wa utawala wa zamani mahakamani, lakini pia wameelezea ukukwaji mkubwa katika mchakato wa kesi hizo.